Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Luka 23:44-56

Luka 23:44-56 NENO

Ilikuwa kama saa sita mchana, nalo giza likafunika nchi yote hadi saa tisa, kwa sababu jua liliacha kutoa nuru. Pazia la Hekalu likachanika vipande viwili. Isa akapaza sauti yake akasema, “Baba, mikononi mwako naikabidhi roho yangu.” Baada ya kusema haya, akakata roho. Yule jemadari alipoona yaliyotukia, akamsifu Mungu, akasema, “Hakika, mtu huyu alikuwa mwenye haki.” Watu wote waliokuwa wamekusanyika hapo kushuhudia tukio hili walipoyaona hayo, wakapigapiga vifua vyao kwa huzuni na kwenda zao. Lakini wale wote waliomfahamu, pamoja na wale wanawake waliokuwa wamemfuata kutoka Galilaya, walisimama kwa mbali wakiyatazama mambo haya. Basi kulikuwa na mtu mmoja mwema na mwenye haki, jina lake Yusufu. Yeye alikuwa mjumbe wa Baraza la Wayahudi, lakini yeye hakuwa amekubaliana na maamuzi na vitendo vya viongozi wenzake. Huyu alikuwa raia wa Arimathaya huko Yudea, naye alikuwa anaungojea ufalme wa Mungu kwa matarajio makubwa. Yusufu alienda kwa Pilato, akaomba apewe mwili wa Isa. Akaushusha kutoka msalabani, akaufunga katika kitambaa cha kitani safi, na kuuweka katika kaburi lililochongwa kwenye mwamba, ambalo halikuwa limezikiwa mtu mwingine bado. Ilikuwa Siku ya Maandalizi, nayo Sabato ilikuwa karibu kuanza. Wale wanawake waliokuwa wamekuja pamoja na Isa wakimfuata kutoka Galilaya wakamfuata Yusufu, wakaliona kaburi na jinsi mwili wa Isa ulivyolazwa. Kisha wakarudi nyumbani, wakaandaa manukato na marhamu ya kuupaka huo mwili. Lakini wakapumzika siku ya Sabato kama ilivyoamriwa.