Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Luka 24:13-35

Luka 24:13-35 NEN

Ikawa siku iyo hiyo, wanafunzi wawili wa Yesu walikuwa njiani wakienda kijiji kilichoitwa Emau, yapata maili saba kutoka Yerusalemu. Walikuwa wakizungumza wao kwa wao kuhusu mambo yote yaliyotukia. Walipokuwa wakizungumza na kujadiliana, Yesu mwenyewe akaja akatembea pamoja nao, lakini macho yao yakazuiliwa ili wasimtambue. Akawauliza, “Ni mambo gani haya mnayozungumza wakati mnatembea?” Wakasimama, nyuso zao zikionyesha huzuni. Mmoja wao, aliyeitwa Kleopa, akamuuliza, “Je, wewe ndiye peke yako mgeni huku Yerusalemu ambaye hufahamu mambo yaliyotukia humo siku hizi?” Akawauliza, “Mambo gani?” Wakamjibu, “Mambo ya Yesu wa Nazareti. Yeye alikuwa nabii, mwenye uwezo mkuu katika maneno yake na matendo yake, mbele za Mungu na mbele ya wanadamu wote. Viongozi wa makuhani na viongozi wetu walimtoa ahukumiwe kufa, nao wakamsulubisha. Lakini tulikuwa tumetegemea kwamba yeye ndiye angelikomboa Israeli. Zaidi ya hayo, leo ni siku ya tatu tangu mambo haya yatokee. Isitoshe, baadhi ya wanawake katika kundi letu wametushtusha. Walikwenda kaburini leo alfajiri, lakini hawakuukuta mwili wake. Walirudi wakasema wameona maono ya malaika ambao waliwaambia kwamba Yesu yu hai. Kisha baadhi ya wenzetu walikwenda kaburini wakalikuta kama vile wale wanawake walivyokuwa wamesema, lakini yeye hawakumwona.” Yesu akawaambia, “Ninyi ni wajinga kiasi gani, nanyi ni wazito mioyoni mwenu kuamini mambo yote yaliyonenwa na manabii! Je, haikumpasa Kristo kuteswa kwa njia hiyo na kisha aingie katika utukufu wake?” Naye akianzia na Sheria ya Mose na Manabii wote, akawafafanulia jinsi Maandiko yalivyosema kumhusu yeye. Nao walipokaribia kile kijiji walichokuwa wakienda, Yesu akawa kama anaendelea mbele. Lakini wao wakamsihi sana akae nao, wakisema, “Kaa hapa nasi, kwa maana sasa ni jioni na usiku unaingia.” Basi akaingia ndani kukaa nao. Alipokuwa mezani pamoja nao, akachukua mkate, akashukuru, akaumega, akaanza kuwagawia. Ndipo macho yao yakafumbuliwa, nao wakamtambua, naye akatoweka machoni pao. Hawakumwona tena. Wakaulizana wao kwa wao, “Je, mioyo yetu haikuwakawaka kwa furaha ndani yetu alipokuwa anazungumza nasi njiani na kutufafanulia Maandiko?” Wakaondoka mara, wakarudi Yerusalemu. Wakawakuta wale wanafunzi kumi na mmoja na wale waliokuwa pamoja nao, wamekusanyika wakisema, “Ni kweli! Bwana amefufuka, naye amemtokea Simoni.” Kisha wale wanafunzi wawili wakaeleza yaliyotukia njiani na jinsi walivyomtambua Yesu alipoumega mkate.