Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Luka 24:13-35

Luka 24:13-35 Biblia Habari Njema (BHN)

Siku hiyohiyo, wawili kati ya wafuasi wake Yesu wakawa wanakwenda katika kijiji kimoja kiitwacho Emau, umbali wa kilomita kumi na moja kutoka Yerusalemu. Wakawa wanazungumza juu ya hayo yote yaliyotukia. Walipokuwa wakizungumza na kujadiliana, Yesu mwenyewe akatokea, akatembea pamoja nao. Walimwona kwa macho, lakini hawakumtambua. Akawauliza, “Mnazungumza nini huku mnatembea?” Nao wakasimama kimya, nyuso zao wamezikunja kwa huzuni. Mmoja, aitwaye Kleopa, akamjibu, “Je, wewe ni mgeni peke yako Yerusalemu ambaye hujui yaliyotukia huko siku hizi?” Naye akawajibu, “Mambo gani?” Wao wakamjibu, “Mambo yaliyompata Yesu wa Nazareti. Yeye alikuwa nabii mwenye uwezo wa kutenda na kufundisha mbele ya Mungu na mbele ya watu wote. Makuhani na watawala wetu walimtoa ahukumiwe kufa, wakamsulubisha. Lakini sisi tulitumaini kwamba yeye ndiye angeikomboa Israeli. Zaidi ya hayo yote, leo ni siku ya tatu tangu mambo hayo yalipotendeka. Tena, wanawake wengine wa kwetu wametushtua. Walikwenda kaburini mapema asubuhi, wasiukute mwili wake. Wakarudi wakasema kwamba walitokewa na malaika waliowaambia kwamba alikuwa hai. Wengine wetu walikwenda kaburini wakashuhudia yale waliyosema hao wanawake; ila yeye hawakumwona.” Kisha Yesu akawaambia, “Mbona mu wapumbavu kiasi hicho na mioyo yenu ni mizito hivyo kusadiki yote yaliyonenwa na manabii? Je, haikumpasa Kristo kuteswa, na hivyo aingie katika utukufu wake?” Akawafafanulia mambo yote yaliyomhusu yeye katika Maandiko Matakatifu kuanzia Mose hadi manabii wote. Walipokikaribia kile kijiji walichokuwa wanakiendea, Yesu akafanya kana kwamba anaendelea na safari; lakini wao wakamsihi wakisema, “Kaa pamoja nasi, maana kunakuchwa, na usiku unakaribia.” Basi, akaingia kijijini, akakaa pamoja nao. Alipoketi kula chakula pamoja nao, akachukua mkate, akaubariki, akaumega, akawapa. Mara macho yao yakafumbuliwa, wakamtambua; lakini yeye akatoweka kati yao. Basi, wakaambiana, “Je, mioyo yetu haikuwa inawaka ndani yetu wakati alipokuwa anatufafanulia Maandiko Matakatifu kule njiani?” Wakaondoka saa ileile, wakarudi Yerusalemu; wakawakuta wale mitume kumi na mmoja na wale wengine waliokuwa pamoja nao wamekusanyika wakisema, “Hakika Bwana amefufuka, amemtokea Simoni.” Basi, hao wafuasi wawili wakawajulisha yale yaliyowapata njiani, na jinsi walivyomtambua katika kumega mkate.

Shirikisha
Soma Luka 24

Luka 24:13-35 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Na tazama, siku ile ile watu wawili miongoni mwao walikuwa wakienda katika kijiji kimoja, jina lake Emau, kilichokuwa mbali na Yerusalemu kama mwendo wa saa mbili. Nao walikuwa wakizungumza wao kwa wao habari za mambo hayo yote yaliyotukia. Ikawa katika kuzungumza na kuulizana kwao, Yesu mwenyewe alikaribia, akaandamana nao. Macho yao yakafumbwa wasimtambue. Akawaambia, Ni maneno gani haya mnayosemezana hivi mnapotembea? Wakasimama wamekunja nyuso zao. Akajibu mmoja wao, jina lake Kleopa, akamwambia, Je! Wewe peke yako u mgeni katika Yerusalemu, hata huyajui yaliyotukia humo siku hizi? Akawauliza, Mambo gani? Wakamwambia, Mambo ya Yesu wa Nazareti, aliyekuwa mtu nabii, mwenye uwezo katika kutenda na kunena mbele za Mungu na watu wote; tena jinsi wakuu wa makuhani na wakubwa wetu walivyomtia katika hukumu ya kufa, wakamsulubisha. Nasi tulikuwa tukitumaini ya kuwa yeye ndiye atakayewakomboa Israeli. Zaidi ya hayo yote, leo ni siku ya tatu tangu yalipotendeka mambo hayo; tena, wanawake kadhaa wa kwetu walitushitusha, waliokwenda kaburini asubuhi na mapema, wasiuone mwili wake; wakaja wakasema ya kwamba wametokewa na malaika waliosema kwamba yu hai. Na wengine waliokuwa pamoja nasi walikwenda kaburini wakaona vivyo hivyo kama wale wanawake walivyosema, ila yeye hawakumwona. Akawaambia, Enyi msiofahamu, wenye mioyo mizito ya kuamini yote waliyoyasema manabii! Je! Haikumpasa Kristo kupata mateso haya na kuingia katika utukufu wake? Akaanza kutoka Musa na manabii wote, akawaeleza katika maandiko yote mambo yaliyomhusu yeye mwenyewe. Wakakikaribia kile kijiji walichokuwa wakienda, naye alifanya kama anataka kuendelea mbele. Wakamshawishi wakisema, Kaa pamoja nasi, kwa kuwa kumekuchwa, na mchana unakwisha. Akaingia ndani kukaa nao. Ikawa alipokuwa ameketi nao chakulani, alitwaa mkate, akaubariki, akaumega, akawapa. Yakafumbuliwa macho yao, wakamtambua; kisha akatoweka mbele yao. Wakaambiana, Je! Mioyo yetu haikuwaka ndani yetu hapo alipokuwa akisema nasi njiani, na kutufunulia Maandiko? Wakaondoka saa ile ile, wakarejea Yerusalemu, wakawakuta wale kumi na mmoja wamekutanika, wao na wale waliokuwa pamoja nao, wakisema, Bwana amefufuka kweli kweli, naye amemtokea Simoni. Nao waliwapa habari ya mambo yale ya njiani, na jinsi alivyotambulikana nao katika kuumega mkate.

Shirikisha
Soma Luka 24

Luka 24:13-35 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Na tazama, siku ile ile watu wawili miongoni mwao walikuwa wakienda kijiji kimoja, jina lake Emau, kilichokuwa mbali na Yerusalemu kama mwendo wa saa mbili. Nao walikuwa wakizungumza wao kwa wao habari za mambo hayo yote yaliyotukia. Ikawa katika kuzungumza na kuulizana kwao, Yesu mwenyewe alikaribia, akaandamana nao. Macho yao yakafumbwa wasimtambue. Akawaambia, Ni maneno gani haya mnayosemezana hivi mnapotembea? Wakasimama wamekunja nyuso zao. Akajibu mmoja wao, jina lake Kleopa, akamwambia, Je! Wewe peke yako u mgeni katika Yerusalemu, hata huyajui yaliyotukia humo siku hizi? Akawauliza, Mambo gani? Wakamwambia, Mambo ya Yesu wa Nazareti, aliyekuwa mtu nabii, mwenye uwezo katika kutenda na kunena mbele za Mungu na watu wote; tena jinsi wakuu wa makuhani na wakubwa wetu walivyomtia katika hukumu ya kufa, wakamsulibisha. Nasi tulikuwa tukitumaini ya kuwa yeye ndiye atakayewakomboa Israeli. Zaidi ya hayo yote, leo ni siku ya tatu tangu yalipotendeka mambo hayo; tena, wanawake kadha wa kadha wa kwetu walitushitusha, waliokwenda kaburini asubuhi na mapema, wasiuone mwili wake; wakaja wakasema ya kwamba wametokewa na malaika waliosema kwamba yu hai. Na wengine waliokuwa pamoja nasi walikwenda kaburini wakaona vivyo hivyo kama wale wanawake walivyosema, ila yeye hawakumwona. Akawaambia, Enyi msiofahamu, wenye mioyo mizito ya kuamini yote waliyoyasema manabii! Je! Haikumpasa Kristo kupata mateso haya na kuingia katika utukufu wake? Akaanza kutoka Musa na manabii wote, akawaeleza katika maandiko yote mambo yaliyomhusu yeye mwenyewe. Wakakikaribia kile kijiji walichokuwa wakienda, naye alifanya kama anataka kuendelea mbele. Wakamshawishi wakisema, Kaa pamoja nasi, kwa kuwa kumekuchwa, na mchana unakwisha. Akaingia ndani kukaa nao. Ikawa alipokuwa ameketi nao chakulani, alitwaa mkate, akaubariki, akaumega, akawapa. Yakafumbuliwa macho yao, wakamtambua; kisha akatoweka mbele yao. Wakaambiana, Je! Mioyo yetu haikuwaka ndani yetu hapo alipokuwa akisema nasi njiani, na kutufunulia maandiko? Wakaondoka saa ile ile, wakarejea Yerusalemu, wakawakuta wale kumi na mmoja wamekutanika, wao na wale waliokuwa pamoja nao, wakisema, Bwana amefufuka kweli kweli, naye amemtokea Simoni. Nao waliwapa habari ya mambo yale ya njiani, na jinsi alivyotambulikana nao katika kuumega mkate.

Shirikisha
Soma Luka 24

Luka 24:13-35 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Ikawa siku iyo hiyo, wanafunzi wawili wa Yesu walikuwa njiani wakienda kijiji kilichoitwa Emau, yapata maili saba kutoka Yerusalemu. Walikuwa wakizungumza wao kwa wao kuhusu mambo yote yaliyotukia. Walipokuwa wakizungumza na kujadiliana, Yesu mwenyewe akaja akatembea pamoja nao, lakini macho yao yakazuiliwa ili wasimtambue. Akawauliza, “Ni mambo gani haya mnayozungumza wakati mnatembea?” Wakasimama, nyuso zao zikionyesha huzuni. Mmoja wao, aliyeitwa Kleopa, akamuuliza, “Je, wewe ndiye peke yako mgeni huku Yerusalemu ambaye hufahamu mambo yaliyotukia humo siku hizi?” Akawauliza, “Mambo gani?” Wakamjibu, “Mambo ya Yesu wa Nazareti. Yeye alikuwa nabii, mwenye uwezo mkuu katika maneno yake na matendo yake, mbele za Mungu na mbele ya wanadamu wote. Viongozi wa makuhani na viongozi wetu walimtoa ahukumiwe kufa, nao wakamsulubisha. Lakini tulikuwa tumetegemea kwamba yeye ndiye angelikomboa Israeli. Zaidi ya hayo, leo ni siku ya tatu tangu mambo haya yatokee. Isitoshe, baadhi ya wanawake katika kundi letu wametushtusha. Walikwenda kaburini leo alfajiri, lakini hawakuukuta mwili wake. Walirudi wakasema wameona maono ya malaika ambao waliwaambia kwamba Yesu yu hai. Kisha baadhi ya wenzetu walikwenda kaburini wakalikuta kama vile wale wanawake walivyokuwa wamesema, lakini yeye hawakumwona.” Yesu akawaambia, “Ninyi ni wajinga kiasi gani, nanyi ni wazito mioyoni mwenu kuamini mambo yote yaliyonenwa na manabii! Je, haikumpasa Kristo kuteswa kwa njia hiyo na kisha aingie katika utukufu wake?” Naye akianzia na Sheria ya Mose na Manabii wote, akawafafanulia jinsi Maandiko yalivyosema kumhusu yeye. Nao walipokaribia kile kijiji walichokuwa wakienda, Yesu akawa kama anaendelea mbele. Lakini wao wakamsihi sana akae nao, wakisema, “Kaa hapa nasi, kwa maana sasa ni jioni na usiku unaingia.” Basi akaingia ndani kukaa nao. Alipokuwa mezani pamoja nao, akachukua mkate, akashukuru, akaumega, akaanza kuwagawia. Ndipo macho yao yakafumbuliwa, nao wakamtambua, naye akatoweka machoni pao. Hawakumwona tena. Wakaulizana wao kwa wao, “Je, mioyo yetu haikuwakawaka kwa furaha ndani yetu alipokuwa anazungumza nasi njiani na kutufafanulia Maandiko?” Wakaondoka mara, wakarudi Yerusalemu. Wakawakuta wale wanafunzi kumi na mmoja na wale waliokuwa pamoja nao, wamekusanyika wakisema, “Ni kweli! Bwana amefufuka, naye amemtokea Simoni.” Kisha wale wanafunzi wawili wakaeleza yaliyotukia njiani na jinsi walivyomtambua Yesu alipoumega mkate.

Shirikisha
Soma Luka 24