Luka 8:40-56
Luka 8:40-56 NENO
Basi Isa aliporudi, umati mkubwa wa watu wakampokea kwa furaha, kwani walikuwa wakimngojea. Kisha mtu mmoja, jina lake Yairo, aliyekuwa kiongozi wa sinagogi, akaja na kuanguka miguuni mwa Isa, akimwomba afike nyumbani mwake, kwa kuwa binti yake wa pekee, mwenye umri wa miaka kumi na mbili, alikuwa anakufa. Isa alipokuwa akienda, umati wa watu wakamsonga sana. Palikuwa na mwanamke mmoja aliyekuwa na tatizo la kutokwa damu kwa muda wa miaka kumi na mbili, [na alikuwa amegharimia mali yake yote kwa matibabu] lakini hakuna yeyote aliyeweza kumponya. Huyo mwanamke akaja kwa nyuma ya Isa na kugusa upindo wa vazi lake. Mara kutokwa damu kwake kukakoma. Isa akauliza, “Ni nani aliyenigusa?” Watu wote walipokana, Petro akasema, “Bwana, umati huu wa watu wanakusonga na kukusukuma kila upande.” Lakini Isa akasema, “Kuna mtu aliyenigusa, kwa maana nimetambua kuwa nguvu zimenitoka.” Yule mwanamke alipofahamu ya kuwa hawezi kuendelea kujificha, alikuja akitetemeka, akaanguka miguuni mwa Isa. Akaeleza mbele ya watu wote kwa nini alimgusa na jinsi alivyoponywa mara moja. Basi Isa akamwambia, “Binti, imani yako imekuponya. Nenda kwa amani.” Isa alipokuwa bado anasema, akaja mtumishi kutoka nyumbani mwa Yairo, yule kiongozi wa sinagogi, kumwambia, “Binti yako amekwisha kufa. Usiendelee kumsumbua Mwalimu.” Isa aliposikia jambo hili, akamwambia Yairo, “Usiogope. Amini tu, naye binti yako atapona.” Walipofika nyumbani mwa Yairo, hakumruhusu mtu yeyote aingie ndani naye isipokuwa Petro, Yohana na Yakobo, pamoja na baba na mama wa yule binti. Wakati ule ule watu wote walikuwa wakilia na kuomboleza kwa ajili ya huyo binti. Isa akawaambia, “Acheni kulia. Huyu binti hajafa, ila amelala.” Wao wakamcheka kwa dharau, wakijua kuwa amekwisha kufa. Isa akamshika yule binti mkono na kuita, “Binti, amka!” Roho yake ikamrudia, naye akainuka mara moja. Akaamuru apewe kitu cha kula. Wazazi wake wakastaajabu sana, lakini Isa akawakataza wasimwambie mtu yeyote kuhusu yale yaliyotukia.