Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Luka 8:40-56

Luka 8:40-56 Biblia Habari Njema (BHN)

Yesu aliporudi upande mwingine wa ziwa, kundi la watu lilimkaribisha, kwa maana wote walikuwa wanamngojea. Hapo akaja mtu mmoja aitwaye Yairo, ofisa wa sunagogi. Alijitupa miguuni pa Yesu, akamwomba aende nyumbani kwake, kwa kuwa binti yake wa pekee, mwenye umri wa miaka kumi na miwili, alikuwa anakufa. Yesu alipokuwa akienda, watu wakawa wanamsonga kila upande. Basi, kulikuwa na mwanamke mmoja kati ya lile kundi la watu, ambaye alikuwa na ugonjwa wa kutokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili; ingawa alikuwa amekwisha tumia mali yake yote kwa waganga, hakuna aliyefaulu kumponya. Huyo mwanamke alimfuata Yesu nyuma, akagusa pindo la vazi lake. Papo hapo akaponywa ugonjwa wake wa kutokwa damu. Yesu akasema, “Ni nani aliyenigusa?” Wote wakasema kwamba hapakuwa na mtu aliyemgusa. Naye Petro akasema, “Bwana, umati wa watu umekuzunguka na kukusonga!” Lakini Yesu akasema, “Kuna mtu aliyenigusa, maana nimehisi nguvu imenitoka.” Yule mwanamke alipoona kwamba hawezi kujificha, akajitokeza akitetemeka kwa hofu, akajitupa mbele ya Yesu. Hapo akaeleza mbele ya wote kisa cha kumgusa Yesu na jinsi alivyoponywa mara moja. Yesu akamwambia, “Binti, imani yako imekuponya. Nenda na amani.” Alipokuwa bado akiongea, Yairo akaletewa habari kutoka nyumbani: “Binti yako amekwisha kufa, ya nini kumsumbua Mwalimu zaidi?” Yesu aliposikia hayo akamwambia Yairo, “Usiogope; amini tu, naye atapona.” Alipofika nyumbani hakumruhusu mtu kuingia ndani pamoja naye, isipokuwa Petro, Yohane, Yakobo na wazazi wa huyo msichana. Watu wote walikuwa wakilia na kuomboleza kwa ajili yake. Lakini Yesu akawaambia, “Msilie, kwa maana mtoto hajafa, amelala tu!” Nao wakamcheka kwa sababu walijua kwamba alikuwa amekufa. Lakini Yesu akamshika mkono akasema, “Mtoto, amka!” Roho yake ikamrudia, akaamka mara. Yesu akaamuru wampe chakula. Wazazi wake walishangaa, lakini Yesu akawaamuru wasimwambie mtu yeyote hayo yaliyotendeka.

Shirikisha
Soma Luka 8

Luka 8:40-56 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Basi Yesu aliporudi mkutano ulimkaribisha kwa furaha, maana wote walikuwa wakimngojea. Na tazama, mtu mmoja akaja, jina lake Yairo, naye ni mtu mkuu wa sinagogi, akaanguka miguuni pa Yesu, akamsihi aingie nyumbani kwake; kwa kuwa binti yake yu karibu kufa, ambaye ni mwana pekee, umri wake amepata miaka kumi na miwili. Na alipokuwa akienda makutano walimsonga. Na mwanamke mmoja, ambaye ametokwa na damu muda wa miaka kumi na miwili, [aliyekuwa amegharimiwa mali zake zote kwa kuwapa waganga] asipate kuponywa na mtu yeyote, alikwenda nyuma yake, akaugusa upindo wa vazi lake; na mara hiyo kutoka damu kwake kulikoma. Yesu akasema, Ni nani aliyenigusa? Basi, watu wote walipokana, Petro alimwambia, Bwana mkubwa, makutano haya wanakuzunguka na kukusonga. Yesu akasema, Mtu alinigusa, maana naona ya kuwa nguvu zimenitoka. Yule mwanamke, alipoona ya kwamba hawezi kusitirika akaja akitetemeka, akaanguka mbele yake, akamweleza mbele ya watu wote sababu yake ya kumgusa, na jinsi alivyoponywa mara moja. Akamwambia, Binti, imani yako imekuponya; nenda zako na amani. Alipokuwa akinena hayo, alikuja mtu kutoka nyumbani kwa yule mkuu wa sinagogi, akamwambia, Binti yako amekwisha kufa; usimsumbue mwalimu. Lakini Yesu aliposikia hayo, alimjibu, Usiwe na hofu, amini tu, naye ataponywa. Alipofika nyumbani hakuruhusu mtu kuingia pamoja naye ila Petro, na Yohana, na Yakobo, na babaye yule mtoto na mamaye. Na watu wote walikuwa wakilia na kumwombolezea; akasema, Msilie, hakufa huyu, bali amelala usingizi tu. Wakamcheka sana, maana walijua ya kuwa amekwisha kufa. Akamshika mkono, akapaza sauti, akisema Kijana, inuka. Roho yake ikamrejea, naye mara hiyo akasimama. Akaamuru apewe chakula. Wazazi wake wakastaajabu sana, lakini akawakataza wasimwambie mtu lililotukia.

Shirikisha
Soma Luka 8

Luka 8:40-56 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Basi Yesu aliporudi mkutano ulimkaribisha kwa furaha, maana walikuwa wakimngojea wote. Na tazama, mtu mmoja akaja, jina lake Yairo, naye ni mtu mkuu wa sinagogi, akaanguka miguuni pa Yesu, akamsihi aingie nyumbani kwake; kwa kuwa binti yake yu katika kufa, ambaye ni mwana pekee, umri wake amepata miaka kumi na miwili. Na alipokuwa akienda makutano walimsonga. Na mwanamke mmoja, ambaye ametokwa na damu muda wa miaka kumi na miwili, [aliyekuwa amegharimiwa mali zake zote kwa kuwapa waganga] asipate kuponywa na mtu ye yote, alikwenda nyuma yake, akaugusa upindo wa vazi lake; na mara hiyo kutoka damu kwake kulikoma. Yesu akasema, Ni nani aliyenigusa? Basi, watu wote walipokana, Petro alimwambia, Bwana mkubwa, makutano haya wanakuzunguka na kukusonga. Yesu akasema, Mtu alinigusa, maana naona ya kuwa nguvu zimenitoka. Yule mwanamke, alipoona ya kwamba hawezi kusitirika akaja akitetemeka, akaanguka mbele yake, akamweleza mbele ya watu wote sababu yake ya kumgusa, na jinsi alivyoponywa mara. Akamwambia Binti, imani yako imekuponya; enenda zako na amani. Alipokuwa akinena hayo, alikuja mtu kutoka nyumbani kwa yule mkuu wa sinagogi, akamwambia, Binti yako amekwisha kufa; usimsumbue mwalimu. Lakini Yesu aliposikia hayo, alimjibu, Usiwe na hofu, amini tu, naye ataponywa. Alipofika nyumbani hakuacha mtu kuingia pamoja naye ila Petro, na Yohana, na Yakobo, na babaye yule mtoto na mamaye. Na watu wote walikuwa wakilia na kumwombolezea; akasema, Msilie, hakufa huyu, bali amelala usingizi tu. Wakamcheka sana, maana walijua ya kuwa amekwisha kufa. Akamshika mkono, akapaza sauti, akisema Kijana, inuka. Roho yake ikamrejea, naye mara hiyo akasimama. Akaamuru apewe chakula. Wazazi wake wakastaajabu sana, lakini akawakataza wasimwambie mtu lililotukia.

Shirikisha
Soma Luka 8

Luka 8:40-56 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)

Basi Isa aliporudi, umati mkubwa wa watu wakampokea kwa furaha, kwani walikuwa wakimngojea. Kisha mtu mmoja, jina lake Yairo, aliyekuwa kiongozi wa sinagogi, akaja na kuanguka miguuni mwa Isa, akimwomba afike nyumbani mwake, kwa kuwa binti yake wa pekee, mwenye umri wa miaka kumi na mbili, alikuwa anakufa. Isa alipokuwa akienda, umati wa watu wakamsonga sana. Palikuwa na mwanamke mmoja aliyekuwa na tatizo la kutokwa damu kwa muda wa miaka kumi na mbili, [na alikuwa amegharimia mali yake yote kwa matibabu] lakini hakuna yeyote aliyeweza kumponya. Huyo mwanamke akaja kwa nyuma ya Isa na kugusa upindo wa vazi lake. Mara kutokwa damu kwake kukakoma. Isa akauliza, “Ni nani aliyenigusa?” Watu wote walipokana, Petro akasema, “Bwana, umati huu wa watu wanakusonga na kukusukuma kila upande.” Lakini Isa akasema, “Kuna mtu aliyenigusa, kwa maana nimetambua kuwa nguvu zimenitoka.” Yule mwanamke alipofahamu ya kuwa hawezi kuendelea kujificha, alikuja akitetemeka, akaanguka miguuni mwa Isa. Akaeleza mbele ya watu wote kwa nini alimgusa na jinsi alivyoponywa mara moja. Basi Isa akamwambia, “Binti, imani yako imekuponya. Nenda kwa amani.” Isa alipokuwa bado anasema, akaja mtumishi kutoka nyumbani mwa Yairo, yule kiongozi wa sinagogi, kumwambia, “Binti yako amekwisha kufa. Usiendelee kumsumbua Mwalimu.” Isa aliposikia jambo hili, akamwambia Yairo, “Usiogope. Amini tu, naye binti yako atapona.” Walipofika nyumbani mwa Yairo, hakumruhusu mtu yeyote aingie ndani naye isipokuwa Petro, Yohana na Yakobo, pamoja na baba na mama wa yule binti. Wakati ule ule watu wote walikuwa wakilia na kuomboleza kwa ajili ya huyo binti. Isa akawaambia, “Acheni kulia. Huyu binti hajafa, ila amelala.” Wao wakamcheka kwa dharau, wakijua kuwa amekwisha kufa. Isa akamshika yule binti mkono na kuita, “Binti, amka!” Roho yake ikamrudia, naye akainuka mara moja. Akaamuru apewe kitu cha kula. Wazazi wake wakastaajabu sana, lakini Isa akawakataza wasimwambie mtu yeyote kuhusu yale yaliyotukia.

Shirikisha
Soma Luka 8