Malaki 2:1-9
Malaki 2:1-9 NENO
“Sasa onyo hili ni kwa ajili yenu, enyi makuhani. Kama hamtasikiliza, na kama hamtaki kuielekeza mioyo yenu kuheshimu Jina langu, nitatuma laana juu yenu, nami nitalaani baraka zenu. Naam, nimekwisha kuzilaani, kwa sababu hamkuielekeza mioyo yenu kuniheshimu mimi,” Asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni. “Kwa sababu yenu nitawakatilia mbali wazao wenu. Nitazipaka nyuso zenu kinyesi, hicho kinyesi cha dhabihu zenu. Nanyi mtafukuzwa pamoja nazo mtoke mbele zangu. Nanyi mtajua kuwa nimewapelekea onyo hili ili agano langu na Lawi lipate kuendelea,” asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni. “Agano langu lilikuwa pamoja naye, agano la uhai na amani, nami nilimpa yote, ili aniche na kuniheshimu, naye akaniheshimu na kusimama akilicha Jina langu. Fundisho la kweli lilikuwa kinywani mwake, wala hakuna uongo wowote uliopatikana katika midomo yake. Alitembea nami katika amani na unyofu, naye akawageuza wengi kutoka dhambini. “Kwa maana yapasa midomo ya kuhani kuhifadhi maarifa. Tena kutoka kinywani mwake watu wangepaswa kutafuta mafundisho, kwa sababu yeye ni mjumbe wa Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni. Lakini mmegeuka mkaiacha njia, na kwa mafundisho yenu mmesababisha wengi kujikwaa. Mmevunja agano na Lawi,” asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni. “Kwa hiyo nimewasababisha ninyi kudharauliwa na kufedheheshwa mbele ya watu wote, kwa sababu hamkufuata njia zangu, bali mmeonesha upendeleo katika mambo ya sheria.”