Mathayo 10
10
Isa achagua mitume kumi na wawili
(Marko 3:13-19; Luka 6:12-16)
1Ndipo Isa akawaita wanafunzi wake kumi na wawili, naye akawapa mamlaka juu ya pepo wachafu, ili waweze kuwatoa na kuponya kila ugonjwa na maradhi ya kila aina.
2Haya ndiyo majina ya hao mitume kumi na wawili:
wa kwanza, Simoni aitwaye Petro, na Andrea nduguye;
Yakobo mwana wa Zebedayo, na Yohana nduguye;
3Filipo, na Bartholomayo;
Tomaso, na Mathayo mtoza ushuru;
Yakobo mwana wa Alfayo, na Thadayo;
4Simoni Mkananayo#10:4 yaani Mzelote; Wazelote walikuwa kikundi cha Kiyahudi wenye imani kali waliompinga Kaisari na utawala wa Rumi., na Yuda Iskariote aliyemsaliti Isa.
Isa awatuma wale kumi na wawili
(Marko 6:7-13; Luka 9:1-6)
5Hawa kumi na wawili, Isa aliwatuma akawaagiza: “Msiende miongoni mwa watu wa Mataifa, wala msiingie mji wowote wa Wasamaria. 6Lakini afadhali mshike njia kuwaendea kondoo wa nyumba ya Israeli waliopotea. 7Mnapoenda, hubirini ujumbe huu, ‘Ufalme wa mbinguni umekaribia.’ 8Ponyeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo wachafu. Mmepata bure, toeni bure. 9Msichukue dhahabu, wala fedha, wala shaba kwenye vifuko vyenu. 10Msichukue mkoba wa safari, wala kanzu mbili, wala jozi ya pili ya viatu, wala fimbo, kwa maana mtendakazi anastahili posho yake.
11“Mji wowote au kijiji chochote mtakapoingia, tafuteni humo mtu anayestahili, nanyi kaeni kwake hadi mtakapoondoka. 12Mkiingia kwenye nyumba, itakieni amani. 13Kama nyumba hiyo inastahili, amani yenu na iwe juu yake. La sivyo, amani yenu na iwarudie ninyi. 14Kama mtu yeyote hatawakaribisha ninyi, wala kusikiliza maneno yenu, kung’uteni mavumbi kutoka miguu yenu mtakapokuwa mnatoka kwenye nyumba hiyo au mji huo. 15Amin, nawaambia, itakuwa rahisi zaidi kwa miji ya Sodoma na Gomora kustahimili katika hukumu kuliko mji huo.
Mateso yanayokuja
(Marko 13:9-13; Luka 21:12-17)
16“Tazama ninawatuma kama kondoo katikati ya mbwa-mwitu. Kwa hiyo mwe werevu kama nyoka na wapole kama hua.
17“Jihadharini na wanadamu; kwa maana watawapeleka katika mabaraza yao na kuwapiga kwenye masinagogi yao. 18Nanyi mtaburutwa mbele ya watawala na wafalme kwa ajili yangu, ili kuwa ushuhuda kwao na kwa watu wa Mataifa. 19Lakini watakapowapeleka humo, msisumbuke kufikiria mtakalosema, kwa maana mtapewa la kusema wakati huo. 20Kwa sababu si ninyi mtakaokuwa mkinena, bali ni Roho wa Baba#10:20 Jina Baba linaonesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu. Kwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu ni Baba kupitia uhusiano unaopatikana katika kumtumaini Isa Al-Masihi. yenu atakayekuwa akinena kupitia kwenu.
21“Ndugu atamsaliti ndugu yake ili auawe, naye baba atamsaliti mtoto wake. Watoto nao wataasi dhidi ya wazazi wao na kusababisha wauawe. 22Watu wote watawachukia kwa ajili ya Jina langu. Lakini yule atakayevumilia hadi mwisho ataokolewa. 23Wakiwatesa katika mji mmoja, kimbilieni mji mwingine. Amin, amin nawaambia, hamtamaliza miji yote ya Israeli kabla Mwana wa Adamu kuja.
24“Mwanafunzi hawezi kumzidi mwalimu wake, wala mtumishi hamzidi bwana wake. 25Yatosha mwanafunzi kuwa kama mwalimu wake, na mtumishi kuwa kama bwana wake. Ikiwa mkuu wa nyumba ameitwa Beelzebuli#10:25 kwa Kiyunani ni Beelzebubu, yaani mkuu wa pepo wachafu, je, si watawaita zaidi wale wa nyumbani mwake!
Maonyo dhidi ya unafiki
(Luka 12:1-12)
26“Basi msiwaogope, kwa maana hakuna kilichofichika ambacho hakitafunuliwa, wala hakuna siri ambayo haitajulikana. 27Ninalowaambia gizani, ninyi lisemeni mchana peupe. Na lile mnalosikia likinong’onwa masikioni mwenu, lihubirini juu ya nyumba. 28Msiwaogope wale wauao mwili lakini hawawezi kuua roho. Afadhali mwogopeni yeye awezaye kuiangamiza roho na mwili katika Jehanamu#10:28 Jehanamu kwa Kiyunani ni Gehena, yaani motoni.. 29Je, shomoro wawili hawauzwi kwa senti moja tu? Lakini hakuna hata mmoja wao atakayeanguka chini pasipo Baba yenu kujua. 30Hata nywele za vichwa vyenu zote zimehesabiwa. 31Hivyo msiogope; kwa maana ninyi ni wa thamani kubwa kuliko shomoro wengi.
32“Kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, mimi nami nitamkiri yeye mbele za Baba yangu aliye mbinguni. 33Lakini yeyote atakayenikana mimi mbele ya watu, mimi nami nitamkana mbele za Baba yangu aliye mbinguni.
Sikuleta amani, bali upanga
(Luka 12:51-53; 14:26-27)
34“Msidhani kwamba nimekuja kuleta amani duniani. Sikuja kuleta amani bali upanga. 35Kwa maana nimekuja kuleta uadui kati ya
“ ‘mtu na baba yake,
binti na mama yake,
mkwe na mama mkwe wake;
36nao adui za mtu watakuwa
ni wale watu wa nyumbani mwake.’#10:36 Mika 7:6
37“Yeyote ampendaye baba yake au mama yake kuliko anavyonipenda mimi, hastahili kuwa wangu. Yeyote ampendaye mwanawe au binti yake kuliko anavyonipenda mimi, hastahili kuwa wangu. 38Tena yeyote asiyeuchukua msalaba wake na kunifuata, hastahili kuwa wangu. 39Kwa maana yeyote anayetaka kuyaokoa maisha yake atayapoteza, lakini yeyote atakayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu atayapata.
Watakaopokea thawabu
(Marko 9:41)
40“Mtu yeyote atakayewapokea ninyi atakuwa amenipokea mimi, na yeyote atakayenipokea mimi atakuwa amempokea yeye aliyenituma. 41Mtu yeyote anayempokea nabii kwa kuwa ni nabii atapokea thawabu ya nabii, naye mtu anayempokea mwenye haki kwa kuwa ni mwenye haki atapokea thawabu ya mwenye haki. 42Mtu yeyote akimpa hata kikombe cha maji baridi mmoja wa hawa wadogo kwa kuwa ni mwanafunzi wangu, amin, nawaambia, hataikosa thawabu yake.”
Iliyochaguliwa sasa
Mathayo 10: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.