Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 11:1-15

Mathayo 11:1-15 NENO

Baada ya Isa kumaliza kutoa maagizo kwa wanafunzi wake kumi na wawili, aliondoka hapo akaenda kufundisha na kuhubiri katika miji ya Galilaya. Yahya aliposikia akiwa gerezani mambo ambayo Al-Masihi alikuwa akiyafanya, aliwatuma wanafunzi wake ili wakamuulize, “Wewe ndiwe yule aliyekuwa aje, au tumngojee mwingine?” Isa akajibu, “Rudini mkamwambie Yahya yale mnayosikia na kuyaona: Vipofu wanapata kuona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, na maskini wanahubiriwa Habari Njema. Amebarikiwa mtu yule asiyechukizwa na mimi.” Wale wanafunzi wa Yahya walipokuwa wanaondoka, Isa akaanza kusema na umati wa watu kuhusu Yahya. Akawauliza, “Mlipoenda kule nyikani, mlienda kuona nini? Je, ni unyasi ukipeperushwa na upepo? Kama sivyo, mlienda kuona nini basi? Mtu aliyevaa mavazi ya kifahari? La hasha! Watu wanaovaa mavazi ya kifahari wako katika majumba ya wafalme. Basi mlienda kuona nini? Mlienda kumwona nabii? Naam, nawaambia, yeye ni zaidi ya nabii. Huyu ndiye ambaye habari zake zimeandikwa: “ ‘Tazama nitamtuma mjumbe wangu mbele yako, atakayetengeneza njia mbele yako.’ Amin, nawaambia, miongoni mwa wale waliozaliwa na wanawake, hajatokea mtu aliye mkuu kuliko Yahya. Lakini aliye mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni ni mkuu kuliko Yahya. Tangu siku za Yahya hadi sasa, ufalme wa mbinguni hunyakuliwa kwa nguvu, nao wenye nguvu wanauteka. Kwa maana manabii wote na Torati walitabiri hadi wakati wa Yahya. Ikiwa mko tayari kukubali hilo, yeye ndiye yule Ilya ambaye manabii walikuwa wamesema angekuja. Yeye aliye na masikio, na asikie.