Mathayo 11:1-15
Mathayo 11:1-15 SRUV
Ikawa Yesu alipokwisha kuwaagiza wanafunzi wake kumi na wawili, alitoka huko kwenda kufundisha na kuhubiri katika miji yao. Naye Yohana aliposikia huko gerezani matendo yake Kristo, alituma wanafunzi wake, kumwuliza, Wewe ndiwe yule ajaye, au tumngojee mwingine? Yesu akajibu akawaambia, Nendeni mkamweleze Yohana mnayoyasikia na kuyaona; vipofu wanapata kuona, viwete wanakwenda, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, na maskini wanahubiriwa Habari Njema. Naye heri awaye yote asiyechukizwa nami. Na hao walipokwenda zao, Yesu alianza kuwaambia makutano habari za Yohana, Mlitoka kwenda nyikani kutazama nini? Unyasi ukitikiswa na upepo? Lakini mlitoka kwenda kuona nini? Mtu aliyevikwa mavazi mororo? Tazama, watu wavaao mavazi mororo wamo katika nyumba za wafalme. Lakini kwa nini mlitoka? Ni kuona nabii? Naam, nawaambia, na aliye mkuu zaidi ya nabii. Huyo ndiye aliyeandikiwa haya, Tazama, mimi namtuma mjumbe wangu Mbele ya uso wako, Atakayeitengeneza njia yako mbele yako. Lakini, nawaambieni, Hajatokea mtu katika wazawa wa wanawake aliye mkuu kuliko Yohana Mbatizaji; lakini aliye mdogo katika ufalme wa mbinguni ni mkuu kuliko yeye. Tangu siku za Yohana Mbatizaji hata sasa ufalme wa mbinguni hupatikana kwa nguvu, nao wenye nguvu huuteka. Kwa maana manabii wote na Torati walitabiri mpaka wakati wa Yohana. Na ikiwa mnataka kukubali, yeye ndiye Eliya atakayekuja. Mwenye masikio, na asikie.