Mathayo 12:1-21
Mathayo 12:1-21 NENO
Wakati huo Isa alipitia kwenye mashamba ya nafaka siku ya Sabato. Wanafunzi wake walikuwa na njaa, nao wakaanza kuvunja masuke ya nafaka na kuyala. Lakini Mafarisayo walipoona jambo hili, wakamwambia, “Tazama! Wanafunzi wako wanafanya jambo lisilo halali kufanywa siku ya Sabato.” Isa akawajibu, “Je, hamjasoma alichofanya Daudi na wenzake walipokuwa na njaa? Aliingia katika nyumba ya Mungu, akala mikate iliyowekwa wakfu, yeye na wenzake, jambo ambalo halikuwa halali kwao kufanya, isipokuwa makuhani tu. Au hamjasoma katika Torati kwamba siku ya Sabato makuhani huvunja sheria ya Sabato Hekaluni lakini hawahesabiwi kuwa na hatia? Nawaambia wazi kwamba, yeye aliye mkuu kuliko Hekalu yupo hapa. Kama mngekuwa mmejua maana ya maneno haya, ‘Nataka rehema, wala si dhabihu,’ msingewalaumu watu wasio na hatia, kwa maana Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa Sabato.” Isa akaondoka mahali hapo, akaingia ndani ya sinagogi lao, na huko alikuwepo mtu aliyepooza mkono. Wakitafuta sababu ya kumshtaki Isa, wakamuuliza, “Je, ni halali kuponya siku ya Sabato?” Isa akawaambia, “Ni nani miongoni mwenu, mwenye kondoo wake ambaye huyo kondoo akitumbukia shimoni siku ya Sabato hatamtoa? Mtu ana thamani kubwa kuliko kondoo. Kwa hiyo ni halali kutenda mema siku ya Sabato.” Ndipo akamwambia yule mtu, “Nyoosha mkono wako.” Akaunyoosha, nao ukaponywa ukawa mzima kama ule mwingine. Lakini Mafarisayo wakatoka nje na kupanga njama ya kumuua Isa. Lakini Isa alipoyatambua mawazo yao, akaondoka mahali hapo. Watu wengi walimfuata, naye akawaponya wote waliokuwa wagonjwa miongoni mwao, akiwakataza wasiseme yeye ni nani, ili neno lililonenwa na nabii Isaya litimie, aliposema: “Tazama mtumishi wangu niliyemchagua, mpendwa wangu, ninayependezwa naye. Nitaweka Roho wangu Mtakatifu juu yake, naye atatangaza haki kwa mataifa. Hatagombana wala kupaza sauti, wala hakuna atakayesikia sauti yake njiani. Mwanzi uliopondeka hatauvunja, na utambi unaofuka moshi hatauzima, hadi atakapoifanya haki ishinde. Katika Jina lake mataifa wataweka tumaini lao.”