Mathayo 12:1-21
Mathayo 12:1-21 Biblia Habari Njema (BHN)
Wakati huo, Yesu alikuwa anapita katika mashamba ya ngano siku ya Sabato. Basi, wanafunzi wake wakaona njaa, wakaanza kukwanyua masuke ya ngano, wakala punje zake. Mafarisayo walipoona hayo, wakamwambia Yesu, “Tazama, wanafunzi wako wanafanya jambo lisilo halali kufanya siku ya Sabato.” Yesu akawajibu, “Je, hamjasoma alivyofanya Daudi pamoja na wenzake wakati walipokuwa na njaa? Yeye aliingia katika nyumba ya Mungu akala ile mikate iliyowekwa mbele ya Mungu. Yeye wala hao wenzake hawakuruhusiwa kula mikate hiyo isipokuwa tu makuhani peke yao. Au je, hamjasoma katika kitabu cha sheria kwamba kila siku ya Sabato makuhani huivunja sheria hekaluni, lakini hawafikiriwi kuwa na hatia? Basi, nawaambieni kwamba hapa pana kikuu kuliko hekalu. Kama tu mngejua maana ya maneno haya: ‘Nataka huruma wala si tambiko,’ hamngewahukumu watu wasio na hatia. Maana Mwana wa Mtu ana uwezo juu ya Sabato.” Yesu alitoka hapo, akaenda katika sunagogi lao. Kulikuwa na mtu mmoja mwenye mkono uliopooza. Basi, watu wakamwuliza Yesu, “Je, ni halali kumponya mtu siku ya Sabato?” Walimwuliza hivyo wapate kisa cha kumshtaki. Lakini Yesu akawaambia, “Tuseme mmoja wenu ana kondoo wake ambaye ametumbukia shimoni; je, hatamshika na kumtoa humo siku ya Sabato? Lakini, mtu ana thamani kuliko kondoo! Basi, ni halali kutenda mema siku ya Sabato.” Kisha akamwambia yule mtu, “Nyosha mkono wako.” Akaunyosha, nao ukawa mzima kabisa kama ule mwingine. Basi, Mafarisayo wakatoka nje, wakashauriana jinsi watakavyomwangamiza Yesu. Lakini Yesu alipojua jambo hilo, akatoka mahali pale. Watu wengi walimfuata, akawaponya wagonjwa wote, akawaamuru wasiwaambie watu habari zake, ili yale aliyosema Mungu kwa njia ya nabii Isaya yatimie: “Tazama mtumishi wangu niliyemteua, mpendwa wangu anipendezaye moyoni. Nitaiweka roho yangu juu yake, naye atatangaza hukumu yangu kwa mataifa yote. Hatakuwa na ubishi wala kupiga kelele, wala sauti yake haitasikika barabarani. Mwanzi uliopondeka hatauvunja, wala utambi ufukao moshi hatauzima, mpaka atakapoifanya hukumu ya haki itawale. Kwake yeye mataifa yatakuwa na matumaini.”
Mathayo 12:1-21 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Wakati ule Yesu alipita katika mashamba siku ya sabato; wanafunzi wake wakaona njaa, wakaanza kuvunja masuke, wakala. Na Mafarisayo walipoona, walimwambia, Tazama! Wanafunzi wako wanafanya jambo ambalo si halali kulifanya siku ya sabato. Akawaambia, Hamkusoma alivyotenda Daudi, alipokuwa na njaa, yeye na wenziwe? Jinsi alivyoingia katika nyumba ya Mungu, akaila mikate ile ya wonyesho, ambayo si halali kwake kuila wala kwa wale wenziwe, ila kwa makuhani peke yao? Wala hamkusoma katika torati, kwamba siku ya sabato makuhani hekaluni huinajisi sabato pasipo kupata hatia? Lakini nawaambieni, kwamba hapa yupo aliye mkuu kuliko hekalu. Lakini kama mngalijua maana yake maneno haya, Nataka rehema, wala si sadaka, msingaliwalaumu wasio na hatia. Kwa maana Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato. Akaondoka huko, akaingia katika sinagogi lao. Na tazama, yumo mtu mwenye mkono umepooza; wakamwuliza, wakisema, Ni halali kuponya watu siku ya sabato? Ili wapate kumshitaki. Akawaambia, Ni mtu yupi miongoni mwenu mwenye kondoo mmoja, na yule kondoo ametumbukia shimoni siku ya sabato, asiyemshika akamwopoa? Je! Mtu ni bora kuliko kondoo mara ngapi? Basi ni halali kutenda mema siku ya sabato. Kisha akamwambia yule mtu, Nyosha mkono wako; akaunyosha, ukapona, ukawa mzima kama ule mwingine. Lakini wale Mafarisayo wakatoka wakafanya shauri juu yake jinsi ya kumwangamiza. Naye Yesu hali akiyafahamu hayo akaondoka huko; na watu wengi wakamfuata; akawaponya wote, akawakataza wasimdhihirishe; ili litimie neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, Tazama, mtumishi wangu niliyemteua; Mpendwa wangu, moyo wangu uliyependezwa naye; Nitatia roho yangu juu yake, Naye atawatangazia Mataifa hukumu. Hatateta wala hatapaza sauti yake; Wala mtu hatasikia sauti yake njiani. Mwanzi uliopondeka hatauvunja, Wala utambi utokao moshi hatauzima, Hadi ailetapo hukumu ikashinda. Na jina lake Mataifa watalitumainia.
Mathayo 12:1-21 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Wakati ule Yesu alipita katika mashamba siku ya sabato; wanafunzi wake wakaona njaa, wakaanza kuvunja masuke, wakala. Na Mafarisayo walipoona, walimwambia, Tazama! Wanafunzi wako wanafanya neno ambalo si halali kulifanya siku ya sabato. Akawaambia, Hamkusoma alivyotenda Daudi, alipokuwa na njaa, yeye na wenziwe? jinsi alivyoingia katika nyumba ya Mungu, akaila mikate ile ya wonyesho, ambayo si halali kwake kuila wala kwa wale wenziwe, ila kwa makuhani peke yao? Wala hamkusoma katika torati, kwamba siku ya sabato makuhani hekaluni huinajisi sabato wasipate hatia? Lakini nawaambieni, kwamba hapa yupo aliye mkuu kuliko hekalu. Lakini kama mngalijua maana yake maneno haya, Nataka rehema, wala si sadaka, msingaliwalaumu wasio na hatia. Kwa maana Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato. Akaondoka huko, akaingia katika sinagogi lao. Na tazama, yumo mtu mwenye mkono umepooza; wakamwuliza, wakisema, Ni halali kuponya watu siku ya sabato? Wapate kumshitaki. Akawaambia, Ni mtu yupi miongoni mwenu mwenye kondoo mmoja, na yule kondoo ametumbukia shimoni siku ya sabato, asiyemshika akamwopoa? Je! Mtu ni bora kuliko kondoo mara ngapi? Basi ni halali kutenda mema siku ya sabato. Kisha akamwambia yule mtu, Nyosha mkono wako; akaunyosha, ukapona, ukawa mzima kama wa pili. Lakini wale Mafarisayo wakatoka wakafanya shauri juu yake jinsi ya kumwangamiza. Naye Yesu hali akiyafahamu hayo akaondoka huko; na watu wengi wakamfuata; akawaponya wote, akawakataza wasimdhihirishe; ili litimie neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, Tazama, mtumishi wangu niliyemteua; Mpendwa wangu, moyo wangu uliyependezwa naye; Nitatia roho yangu juu yake, Naye atawatangazia Mataifa hukumu. Hatateta wala hatapaza sauti yake; Wala mtu hatasikia sauti yake njiani. Mwanzi uliopondeka hatauvunja, Wala utambi utokao moshi hatauzima, Hata ailetapo hukumu ikashinda. Na jina lake Mataifa watalitumainia.
Mathayo 12:1-21 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Wakati huo Isa alipitia kwenye mashamba ya nafaka siku ya Sabato. Wanafunzi wake walikuwa na njaa, nao wakaanza kuvunja masuke ya nafaka na kuyala. Lakini Mafarisayo walipoona jambo hili, wakamwambia, “Tazama! Wanafunzi wako wanafanya jambo lisilo halali kufanywa siku ya Sabato.” Isa akawajibu, “Je, hamjasoma alichofanya Daudi na wenzake walipokuwa na njaa? Aliingia katika nyumba ya Mungu, akala mikate iliyowekwa wakfu, yeye na wenzake, jambo ambalo halikuwa halali kwao kufanya, isipokuwa makuhani tu. Au hamjasoma katika Torati kwamba siku ya Sabato makuhani huvunja sheria ya Sabato Hekaluni lakini hawahesabiwi kuwa na hatia? Nawaambia wazi kwamba, yeye aliye mkuu kuliko Hekalu yupo hapa. Kama mngekuwa mmejua maana ya maneno haya, ‘Nataka rehema, wala si dhabihu,’ msingewalaumu watu wasio na hatia, kwa maana Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa Sabato.” Isa akaondoka mahali hapo, akaingia ndani ya sinagogi lao, na huko alikuwepo mtu aliyepooza mkono. Wakitafuta sababu ya kumshtaki Isa, wakamuuliza, “Je, ni halali kuponya siku ya Sabato?” Isa akawaambia, “Ni nani miongoni mwenu, mwenye kondoo wake ambaye huyo kondoo akitumbukia shimoni siku ya Sabato hatamtoa? Mtu ana thamani kubwa kuliko kondoo. Kwa hiyo ni halali kutenda mema siku ya Sabato.” Ndipo akamwambia yule mtu, “Nyoosha mkono wako.” Akaunyoosha, nao ukaponywa ukawa mzima kama ule mwingine. Lakini Mafarisayo wakatoka nje na kupanga njama ya kumuua Isa. Lakini Isa alipoyatambua mawazo yao, akaondoka mahali hapo. Watu wengi walimfuata, naye akawaponya wote waliokuwa wagonjwa miongoni mwao, akiwakataza wasiseme yeye ni nani, ili neno lililonenwa na nabii Isaya litimie, aliposema: “Tazama mtumishi wangu niliyemchagua, mpendwa wangu, ninayependezwa naye. Nitaweka Roho wangu Mtakatifu juu yake, naye atatangaza haki kwa mataifa. Hatagombana wala kupaza sauti, wala hakuna atakayesikia sauti yake njiani. Mwanzi uliopondeka hatauvunja, na utambi unaofuka moshi hatauzima, hadi atakapoifanya haki ishinde. Katika Jina lake mataifa wataweka tumaini lao.”