Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 13:24-43

Mathayo 13:24-43 NEN

Yesu akawaambia mfano mwingine, akasema: “Ufalme wa Mbinguni unaweza kufananishwa na mtu aliyepanda mbegu nzuri katika shamba lake. Lakini wakati kila mtu alipokuwa amelala, adui yake akaja na kupanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake. Ngano ilipoota na kutoa masuke, magugu nayo yakatokea. “Watumishi wa yule mwenye shamba wakamjia na kumwambia, ‘Bwana, si tulipanda mbegu nzuri shambani mwako? Basi, magugu yametoka wapi?’ “Akawajibu, ‘Adui ndiye alifanya jambo hili.’ “Wale watumishi wakamuuliza, ‘Je, unataka twende tukayangʼoe?’ “Lakini akasema, ‘Hapana, msiyangʼoe, kwa maana wakati mkingʼoa magugu mnaweza mkangʼoa na ngano pamoja nayo. Acheni ngano na magugu vikue vyote pamoja mpaka wakati wa mavuno. Wakati huo nitawaambia wavunaji wayakusanye magugu kwanza, wayafunge matita matita ili yachomwe moto; kisha wakusanye ngano na kuileta ghalani mwangu.’ ” Akawaambia mfano mwingine, akasema, “Ufalme wa Mbinguni ni kama punje ya haradali, ambayo mtu aliichukua, akaipanda shambani mwake. Ingawa mbegu hiyo ni ndogo kuliko mbegu zote, lakini inapokua ni mmea mkubwa kuliko yote ya bustanini, nao huwa mti mkubwa, hadi ndege wa angani wanakuja na kutengeneza viota katika matawi yake.” Akawaambia mfano mwingine, “Ufalme wa Mbinguni unafanana na chachu ambayo mwanamke aliichukua akaichanganya katika kiasi kikubwa cha unga mpaka wote ukaumuka.” Yesu alinena mambo haya yote kwa makutano kwa mifano. Wala hakuwaambia lolote pasipo mfano. Hii ilikuwa ili kutimiza lile lililonenwa kwa kinywa cha nabii aliposema: “Nitafungua kinywa changu niseme nao kwa mifano; nitahubiri mambo yaliyofichika tangu kuumbwa kwa misingi ya ulimwengu.” Kisha Yesu akaagana na makutano, akaingia nyumbani. Wanafunzi wake wakamjia wakamwambia, “Tueleze maana ya ule mfano wa magugu shambani.” Akawaambia, “Aliyepanda mbegu nzuri ni Mwana wa Adamu. Shamba ni ulimwengu na mbegu nzuri ni wana wa Ufalme. Magugu ni wana wa yule mwovu. Yule adui aliyepanda magugu ni ibilisi. Mavuno ni mwisho wa dunia, nao wavunaji ni malaika. “Kama vile magugu yangʼolewavyo na kuchomwa motoni, ndivyo itakavyokuwa wakati wa mwisho wa dunia. Mwana wa Adamu atawatuma malaika zake, nao watakusanya kutoka Ufalme wake kila kitu kinachosababisha dhambi na watenda maovu wote. Nao watawatupa katika tanuru la moto ambako kutakuwa na kilio na kusaga meno. Ndipo wenye haki watangʼaa kama jua katika Ufalme wa Baba yao. Yeye aliye na masikio, na asikie.

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Mathayo 13:24-43