Mathayo 20:1-16
Mathayo 20:1-16 NEN
“Kwa maana Ufalme wa Mbinguni unafanana na mtu mwenye shamba aliyetoka alfajiri ili kwenda kuajiri vibarua kufanya kazi katika shamba lake la mizabibu. Baada ya kukubaliana na hao vibarua kuwalipa ujira wa dinari moja kwa siku, akawapeleka kwenye shamba lake la mizabibu. “Mnamo saa tatu akatoka tena, akawakuta wengine wamesimama sokoni bila kazi. Akawaambia, ‘Ninyi nanyi nendeni mkafanye kazi katika shamba langu la mizabibu, nami nitawalipa chochote kilicho haki yenu.’ Kwa hiyo wakaenda. “Akatoka tena mnamo saa sita na pia saa tisa akafanya vivyo hivyo. Mnamo saa kumi na moja akatoka tena akawakuta wengine bado wamesimama bila kazi. Akawauliza, ‘Kwa nini mmesimama hapa kutwa nzima pasipo kufanya kazi?’ “Wakamjibu, ‘Ni kwa sababu hakuna yeyote aliyetuajiri.’ “Akawaambia, ‘Ninyi nanyi nendeni mkafanye kazi katika shamba langu la mizabibu.’ “Ilipofika jioni, yule mwenye shamba la mizabibu akamwambia msimamizi, ‘Waite hao vibarua na uwalipe ujira wao, ukianzia na wale walioajiriwa mwisho na kuishia na wale walioajiriwa kwanza.’ “Wale vibarua walioajiriwa mnamo saa kumi na moja, wakaja na kila mmoja wao akapokea dinari moja. Hivyo wale walioajiriwa kwanza walipofika, walidhani watalipwa zaidi. Lakini kila mmoja wao pia alipokea dinari moja. Walipoipokea, wakaanza kulalamika dhidi ya yule mwenye shamba, wakisema, ‘Hawa watu walioajiriwa mwisho wamefanya kazi kwa muda wa saa moja tu, nawe umewafanya sawa na sisi ambao tumestahimili taabu na joto lote la mchana kutwa?’ “Yule mwenye shamba akamjibu mmoja wao, ‘Rafiki, sijakudhulumu. Je, hukukubaliana nami kwa ujira wa kawaida wa dinari moja? Chukua ujira wako na uende. Mimi nimeamua kumlipa huyu mtu aliyeajiriwa mwisho kama nilivyokupa wewe. Je, sina haki yangu kufanya kile nitakacho na mali yangu mwenyewe? Au unaona wivu kwa kuwa nimekuwa mkarimu?’ “Vivyo hivyo, wa mwisho watakuwa wa kwanza, na wa kwanza watakuwa wa mwisho.”