Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 20:17-28

Mathayo 20:17-28 NENO

Basi Isa alipokuwa anapanda kwenda Yerusalemu, aliwaita kando wale wanafunzi kumi na wawili na kuwaambia, “Tunapanda kwenda Yerusalemu, na Mwana wa Adamu atatiwa mikononi mwa viongozi wa makuhani na walimu wa Torati. Nao watamhukumu kifo na kumtia mikononi mwa watu wa Mataifa ili wamdhihaki na kumpiga mijeledi na kumsulubisha msalabani. Naye atafufuliwa siku ya tatu!” Kisha mama yao wana wa Zebedayo akamjia Isa pamoja na wanawe, naye akapiga magoti mbele yake, akamwomba Isa amfanyie jambo fulani. Isa akamuuliza, “Unataka nini?” Akajibu, “Tafadhali, wajalie wanangu hawa ili mmoja aketi upande wako wa kuume, na mwingine upande wako wa kushoto katika ufalme wako.” Isa akawaambia, “Ninyi hamjui mnaloliomba. Je, mnaweza kukinywea kikombe nitakachonywea mimi?” Wakajibu, “Tunaweza.” Isa akawaambia, “Kwa kweli kikombe changu mtakinywea, lakini kuketi upande wangu wa kuume au wa kushoto si langu mimi kuwapa. Nafasi hizo ni za wale ambao wameandaliwa na Baba yangu.” Wale wanafunzi wengine kumi waliposikia haya, waliwakasirikia hao ndugu wawili. Lakini Isa akawaita wote pamoja na kuwaambia, “Mnafahamu kuwa watawala wa watu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, nao wenye vyeo huonesha mamlaka yao. Isiwe hivyo kwenu. Badala yake, yeyote anayetaka kuwa mkuu miongoni mwenu hana budi kuwa mtumishi wenu, naye anayetaka kuwa wa kwanza miongoni mwenu hana budi kuwa mtumwa wenu: kama vile Mwana wa Adamu hakuja kutumikiwa, bali kutumika na kuutoa uhai wake uwe fidia kwa ajili ya wengi.”