Mathayo 21:12-22
Mathayo 21:12-22 NENO
Isa akaingia katika eneo la Hekalu na kuwafukuza wote waliokuwa wakinunua na kuuza vitu Hekaluni. Akazipindua meza za wale waliokuwa wakibadilisha fedha, na pia viti vya wale waliokuwa wakiuza njiwa. Akawaambia, “Imeandikwa, ‘Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala,’ lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang’anyi.” Vipofu na vilema wakamwendea kule Hekaluni, naye akawaponya. Lakini viongozi wa makuhani na walimu wa Torati walipoona mambo ya ajabu aliyofanya, na kuwasikia watoto wakishangilia katika eneo la Hekalu, wakisema, “Hosana Mwana wa Daudi,” walikasirika. Wakamuuliza Isa, “Je, unasikia hayo hawa wanayosema?” Akawajibu, “Naam; kwani hamkusoma, “ ‘Midomoni mwa watoto wachanga na wanaonyonya umeamuru sifa’?” Akawaacha, akatoka nje ya mji, akaenda hadi Bethania, akalala huko. Asubuhi na mapema, Isa alipokuwa akirudi mjini, alikuwa na njaa. Akauona mtini kando ya barabara, naye akaukaribia, lakini hakupata tunda lolote ila majani. Ndipo akauambia, “Wewe usizae matunda tena kamwe!” Papo hapo ule mtini ukanyauka. Wanafunzi wake walipoona jambo hili, wakashangaa, wakamuuliza, “Imekuwaje mtini huu kunyauka ghafula?” Isa akawajibu, “Amin, nawaambia, mkiwa na imani wala msiwe na shaka, si kwamba mtaweza kufanya tu yale yaliyofanyika kwa huu mtini, bali hata mkiuambia huu mlima, ‘Ng’oka, ukatupwe baharini,’ litafanyika. Yoyote mtakayoyaomba mkisali na mkiamini, mtayapokea.”