Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 21:12-22

Mathayo 21:12-22 Biblia Habari Njema (BHN)

Basi, Yesu akaingia hekaluni, akawafukuza nje watu waliokuwa wanauza na kununua vitu ndani ya hekalu; akazipindua meza za wale waliokuwa wanavunja fedha, na viti vya wale waliokuwa wanauza njiwa. Akawaambia, “Imeandikwa katika Maandiko Matakatifu: ‘Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala.’ Lakini nyinyi mmeifanya kuwa pango la wanyanganyi.” Vipofu na vilema wengine walimwendea huko hekaluni, naye Yesu akawaponya. Basi, makuhani wakuu na waalimu wa sheria walipoyaona maajabu aliyoyafanya Yesu, na pia watoto walipokuwa wanapaza sauti zao hekaluni wakisema: “Sifa kwa Mwana wa Daudi,” wakakasirika. Hivyo wakamwambia, “Je, husikii wanachosema?” Yesu akawajibu, “Naam, nasikia! Je hamjapata kusoma Maandiko haya? ‘Kwa vinywa vya watoto wadogo na wachanga wajipatia sifa kamili.’” Basi, akawaacha, akatoka nje ya mji na kwenda Bethania, akalala huko. Yesu alipokuwa anarudi mjini asubuhi na mapema, aliona njaa. Akauona mtini mmoja kando ya njia, akauendea; lakini aliukuta hauna chochote ila majani matupu. Basi, akauambia, “Usizae tena matunda milele!” Papo hapo huo mtini ukanyauka. Wanafunzi walipouona walishangaa wakisema, “Kwa nini mtini huu umenyauka ghafla?” Yesu akawajibu, “Kweli nawaambieni, kama mkiwa na imani bila kuwa na mashaka, mnaweza si tu kufanya hivyo, bali hata mkiuambia mlima huu: ‘Ngoka ukajitose baharini,’ itafanyika hivyo. Na mkiwa na imani, chochote mtakachoomba kwa sala, mtapata.”

Shirikisha
Soma Mathayo 21

Mathayo 21:12-22 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)

Isa akaingia katika eneo la Hekalu na kuwafukuza wote waliokuwa wakinunua na kuuza vitu Hekaluni. Akazipindua meza za wale waliokuwa wakibadilisha fedha, na pia viti vya wale waliokuwa wakiuza njiwa. Akawaambia, “Imeandikwa, ‘Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala,’ lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang’anyi.” Vipofu na vilema wakamwendea kule Hekaluni, naye akawaponya. Lakini viongozi wa makuhani na walimu wa Torati walipoona mambo ya ajabu aliyofanya, na kuwasikia watoto wakishangilia katika eneo la Hekalu, wakisema, “Hosana Mwana wa Daudi,” walikasirika. Wakamuuliza Isa, “Je, unasikia hayo hawa wanayosema?” Akawajibu, “Naam; kwani hamkusoma, “ ‘Midomoni mwa watoto wachanga na wanaonyonya umeamuru sifa’?” Akawaacha, akatoka nje ya mji, akaenda hadi Bethania, akalala huko. Asubuhi na mapema, Isa alipokuwa akirudi mjini, alikuwa na njaa. Akauona mtini kando ya barabara, naye akaukaribia, lakini hakupata tunda lolote ila majani. Ndipo akauambia, “Wewe usizae matunda tena kamwe!” Papo hapo ule mtini ukanyauka. Wanafunzi wake walipoona jambo hili, wakashangaa, wakamuuliza, “Imekuwaje mtini huu kunyauka ghafula?” Isa akawajibu, “Amin, nawaambia, mkiwa na imani wala msiwe na shaka, si kwamba mtaweza kufanya tu yale yaliyofanyika kwa huu mtini, bali hata mkiuambia huu mlima, ‘Ng’oka, ukatupwe baharini,’ litafanyika. Yoyote mtakayoyaomba mkisali na mkiamini, mtayapokea.”

Shirikisha
Soma Mathayo 21