Mathayo 23:1-12
Mathayo 23:1-12 NEN
Kisha Yesu akauambia umati wa watu pamoja na wanafunzi wake: “Walimu wa sheria na Mafarisayo wameketi katika kiti cha Mose, hivyo inawapasa kuwatii na kufanya kila kitu wanachowaambia. Lakini msifuate yale wanayotenda, kwa sababu hawatendi yale wanayohubiri. Wao hufunga mizigo mikubwa na kuiweka mabegani mwa watu, lakini wao wenyewe hawako radhi hata kuinua kidole ili kuisogeza. “Wao hutenda mambo yao yote ili waonekane na watu. Hupanua vikasha vyao vyenye maandiko ya sheria na kurefusha matamvua ya mavazi yao. Wanapenda kukalia viti vya heshima katika karamu, na vile viti maalum sana katika masinagogi. Hupenda kusalimiwa masokoni na kutaka watu wawaite ‘Rabi.’ “Lakini ninyi msiitwe ‘Rabi,’ kwa sababu mnaye Bwana mmoja na ninyi nyote ni ndugu. Nanyi msimwite mtu yeyote ‘Baba,’ hapa duniani, kwa maana mnaye Baba mmoja, naye yuko mbinguni. Wala msiitwe ‘Mwalimu,’ kwa maana mnaye mwalimu mmoja tu, ndiye Kristo. Yeye aliye mkuu kuliko ninyi nyote miongoni mwenu atakuwa mtumishi wenu. Kwa kuwa yeyote anayejikweza atashushwa, na yeyote anayejinyenyekeza atakwezwa.