Mathayo 24:15-28
Mathayo 24:15-28 NENO
“Hivyo mtakapoona lile ‘chukizo la uharibifu’ lililonenwa na nabii Danieli limesimama mahali patakatifu (asomaye na afahamu), basi wale walio Yudea wakimbilie milimani. Yeyote aliye juu ya dari ya nyumba asishuke ili kuchukua chochote kutoka ndani ya nyumba. Aliye shambani asirudi nyumbani kuchukua vazi lake. Ole wao wenye mimba na wale wanaonyonyesha watoto siku hizo! Ombeni ili kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi au siku ya Sabato. Kwa maana wakati huo kutakuwa na dhiki kuu ambayo haijapata kuwepo tangu mwanzo wa dunia hadi sasa: wala haitakuwepo tena kamwe. “Kama siku hizo zisingefupishwa, hakuna mtu ambaye angeokoka. Lakini kwa ajili ya wateule, siku hizo zitafupishwa. Wakati huo mtu yeyote akiwaambia, ‘Tazama, Al-Masihi huyu hapa!’ au, ‘Al-Masihi yuko kule,’ msisadiki. Kwa maana watatokea masihi wa uongo na manabii wa uongo, nao watafanya ishara kubwa na maajabu mengi ili kuwapotosha, ikiwezekana, hata wale wateule hasa. Tazameni, nimekwisha kuwaambia mapema. “Basi mtu yeyote akiwaambia, ‘Yule kule nyikani,’ msiende huko. Au akisema, ‘Yuko kwenye chumba,’ msisadiki. Kwa maana kama vile radi itokavyo mashariki na kuonekana hata magharibi, ndivyo itakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. Kwa maana popote ulipo mzoga, huko ndiko wakusanyikapo tai.