Mathayo 24
24
Unabii kuhusu mambo yajayo
(Mathayo 24–25)
Kubomolewa kwa Hekalu kwatabiriwa
(Marko 13:1-2; Luka 21:5-6)
1Isa akatoka Hekaluni na alipokuwa akienda zake, wanafunzi wake wakamwendea ili kumwonesha majengo ya Hekalu. 2Ndipo Isa akawauliza, “Je, mnayaona haya yote? Amin, nawaambia, hakuna hata jiwe moja hapa litakalobaki juu ya jingine, bali kila moja litabomolewa.”
Ishara za nyakati za mwisho
(Marko 13:3-23; Luka 21:7-24)
3Isa alipokuwa ameketi kwenye Mlima wa Mizeituni, wanafunzi wake wakamjia faraghani, wakamuuliza, “Tuambie, mambo haya yatatukia lini, nayo dalili ya kuja kwako na ya mwisho wa dunia ni gani?”
4Isa akawajibu, “Jihadharini, mtu yeyote asiwadanganye. 5Kwa maana wengi watakuja kwa Jina langu, wakidai, ‘Mimi ndiye Al-Masihi#24:5 Al-Masihi maana yake Aliyetiwa mafuta.,’ nao watawadanganya wengi. 6Mtasikia habari za vita na tetesi za vita. Angalieni msitishike, kwa maana haya hayana budi kutukia. Lakini ule mwisho bado. 7Taifa litainuka dhidi ya taifa, na ufalme dhidi ya ufalme. Kutakuwa na njaa na mitetemeko ya ardhi sehemu mbalimbali. 8Haya yote yatakuwa ndio mwanzo wa uchungu.
9“Ndipo mtasalitiwa, ili mteswe na kuuawa, nanyi mtachukiwa na mataifa yote kwa ajili yangu. 10Wakati huo, wengi wataacha imani yao, nao watasalitiana kila mmoja na mwenzake na kuchukiana. 11Watatokea manabii wengi wa uongo, nao watawadanganya watu wengi. 12Kwa sababu ya kuongezeka kwa uovu, upendo wa watu wengi utapoa, 13lakini yule atakayevumilia hadi mwisho ataokolewa. 14Injili hii ya ufalme itahubiriwa ulimwenguni kote kuwa ushuhuda kwa mataifa yote. Ndipo mwisho utakapokuja.
Chukizo la uharibifu
(Marko 13:14-23; Luka 21:20-24)
15“Hivyo mtakapoona lile ‘chukizo la uharibifu’#24:15 Danieli 9:27; 11:31; 12:11 lililonenwa na nabii Danieli limesimama mahali patakatifu (asomaye na afahamu), 16basi wale walio Yudea wakimbilie milimani. 17Yeyote aliye juu ya dari ya nyumba asishuke ili kuchukua chochote kutoka ndani ya nyumba. 18Aliye shambani asirudi nyumbani kuchukua vazi lake. 19Ole wao wenye mimba na wale wanaonyonyesha watoto siku hizo! 20Ombeni ili kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi au siku ya Sabato. 21Kwa maana wakati huo kutakuwa na dhiki kuu ambayo haijapata kuwepo tangu mwanzo wa dunia hadi sasa: wala haitakuwepo tena kamwe.
22“Kama siku hizo zisingefupishwa, hakuna mtu ambaye angeokoka. Lakini kwa ajili ya wateule, siku hizo zitafupishwa. 23Wakati huo mtu yeyote akiwaambia, ‘Tazama, Al-Masihi huyu hapa!’ au, ‘Al-Masihi yuko kule,’ msisadiki. 24Kwa maana watatokea masihi wa uongo na manabii wa uongo, nao watafanya ishara kubwa na maajabu mengi ili kuwapotosha, ikiwezekana, hata wale wateule hasa. 25Tazameni, nimekwisha kuwaambia mapema.
26“Basi mtu yeyote akiwaambia, ‘Yule kule nyikani,’ msiende huko. Au akisema, ‘Yuko kwenye chumba,’ msisadiki. 27Kwa maana kama vile radi itokavyo mashariki na kuonekana hata magharibi, ndivyo itakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. 28Kwa maana popote ulipo mzoga, huko ndiko wakusanyikapo tai.
Kuja kwa Mwana wa Adamu
(Marko 13:24-31; Luka 21:25-33)
29“Mara baada ya dhiki ya siku zile,
“ ‘jua litatiwa giza,
nao mwezi hautatoa nuru yake;
nazo nyota zitaanguka kutoka angani,
na nguvu za anga zitatikisika.’#24:29 Isaya 13:10; 34:4
30“Ndipo itakapotokea ishara ya Mwana wa Adamu angani, na makabila yote ya dunia yataomboleza. Nao watamwona Mwana wa Adamu akija juu ya mawingu ya angani, katika uwezo na utukufu mkuu. 31Naye atawatuma malaika wake kwa sauti kuu ya tarumbeta, nao watawakusanya wateule wake kutoka pande zote nne za dunia, kutoka mwisho mmoja wa mbingu hadi mwisho mwingine.
Somo kuhusu mtini
(Marko 13:28-31; Luka 21:29-33)
32“Basi jifunzeni somo hili kutokana na mtini: Matawi yake yanapoanza kuchipua na kutoa majani, mnatambua kwamba wakati wa kiangazi umekaribia. 33Vivyo hivyo, mnapoyaona mambo haya yote, mtambue kwamba wakati u karibu, hata malangoni. 34Amin, nawaambia, kizazi hiki hakitapita hadi mambo haya yote yawe yametimia. 35Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.
Hakuna ajuaye siku wala saa
(Marko 13:32-37; Luka 17:26-30, 34-36)
36“Kwa habari ya siku ile na saa, hakuna ajuaye, hata malaika walio mbinguni wala Mwana, ila Baba#24:36 Jina Baba linaonesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu. Kwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu ni Baba kupitia uhusiano unaopatikana katika kumtumaini Isa Al-Masihi. peke yake. 37Kama ilivyokuwa wakati wa Nuhu, ndivyo itakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. 38Kwa maana siku zile kabla ya gharika, watu walikuwa wakila na kunywa, wakioa na kuolewa, hadi siku ile Nuhu alipoingia katika safina. 39Nao hawakujua lolote hadi gharika ilipokuja ikawakumba wote. Hivyo ndivyo itakavyokuwa atakapokuja Mwana wa Adamu. 40Watu wawili watakuwa shambani, naye mmoja atatwaliwa na mwingine ataachwa. 41Wanawake wawili watakuwa wanasaga kwa kinu cha mkono, naye mmoja atatwaliwa na mwingine ataachwa.
42“Basi kesheni, kwa sababu hamjui ni siku gani atakapokuja Bwana wenu. 43Lakini fahamuni jambo hili: Kama mwenye nyumba angejua ni wakati gani wa usiku ambao mwizi atakuja, angekesha na hangekubali nyumba yake kuvunjwa. 44Kwa hiyo ninyi pia hamna budi kuwa tayari, kwa sababu Mwana wa Adamu atakuja saa msiyotazamia.
Mfano wa mtumishi mwaminifu
(Luka 12:41-48)
45“Ni nani basi aliye mtumishi mwaminifu na mwenye busara, ambaye bwana wake amemweka kusimamia watumishi wengine katika nyumba yake, ili awape chakula chao kwa wakati unaofaa? 46Heri mtumishi yule ambaye bwana wake atakaporudi atamkuta akifanya hivyo. 47Amin, nawaambia, atamweka mtumishi huyo kuwa msimamizi wa mali yake yote. 48Lakini kama huyo mtumishi ni mwovu, naye akasema moyoni mwake, ‘Bwana wangu atakawia muda mrefu,’ 49kisha akaanza kuwapiga watumishi wenzake, na kula na kunywa pamoja na walevi. 50Basi bwana wa mtumishi huyo atakuja siku asiyodhani na saa asiyoijua. 51Atamkata vipande vipande na kumweka pamoja na wanafiki, mahali ambako kutakuwa ni kulia na kusaga meno.
Iliyochaguliwa sasa
Mathayo 24: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.