Mathayo 23
23
Isa atahadharisha kuhusu walimu wa Torati
(Marko 12:38-40; Luka 11:39-52; 20:45-47)
1Kisha Isa akaambia wale umati wa watu na wanafunzi wake: 2“Walimu wa Torati na Mafarisayo wameketi kwenye kiti cha Musa, 3hivyo inawapasa kuwatii na kufanya kila kitu wanachowaambia. Lakini msifuate yale wanayotenda, kwa sababu hawatendi yale wanayohubiri. 4Wao hufunga mizigo mikubwa na kuiweka mabegani mwa watu, lakini wao wenyewe hawako radhi hata kuinua kidole ili kuisogeza.
5“Wao hutenda mambo yao yote ili waonekane na watu. Hupanua vikasha vyao vyenye maandiko ya sheria na kurefusha matamvua ya mavazi yao. 6Wanapenda kukalia viti vya heshima katika karamu, na vile viti maalum sana katika masinagogi#23:6 Nyumba za ibada na mafunzo.. 7Hupenda kusalimiwa masokoni na kutaka watu wawaite ‘Mwalimu.’
8“Lakini ninyi msiitwe ‘Mwalimu,’ kwa sababu mnaye Bwana mmoja na ninyi nyote ni ndugu. 9Nanyi msimwite mtu yeyote ‘Baba,’ hapa duniani, kwa maana mnaye Baba#23:9 Jina Baba linaonesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu. Kwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu ni Baba kupitia uhusiano unaopatikana katika kumtumaini Isa Al-Masihi. mmoja, naye yuko mbinguni. 10Wala msiitwe ‘Mwalimu,’ kwa maana mnaye mwalimu mmoja tu, ndiye Al-Masihi#23:10 Al-Masihi maana yake Aliyetiwa mafuta.. 11Yeye aliye mkuu kuliko ninyi nyote miongoni mwenu atakuwa mtumishi wenu. 12Kwa kuwa yeyote anayejikweza atashushwa, na yeyote anayejinyenyekeza atakwezwa.
Ole saba kwa walimu wa Torati na Mafarisayo
13“Lakini ole wenu, walimu wa Torati na Mafarisayo, enyi wanafiki! Kwa maana mnawafungia watu milango ya ufalme wa mbinguni. Ninyi wenyewe hamuingii humo, nao wale wanaotaka kuingia mnawazuia. [ 14Ole wenu walimu wa Torati na Mafarisayo, enyi wanafiki! Mnakula katika nyumba za wajane, nanyi kwa kujifanya kuwa wema, mnasali sala ndefu. Kwa hiyo hukumu yenu itakuwa kuu zaidi.]#23:14 Maandiko mengine ya kale hayana maneno haya.
15“Ole wenu walimu wa Torati na Mafarisayo, enyi wanafiki! Ninyi mnasafiri baharini na nchi kavu ili kumfanya mtu mmoja mwongofu, lakini baada ya kumpata, mnamfanya mwana wa Jehanamu mara mbili kuliko ninyi!
16“Ole wenu, viongozi vipofu! Ninyi mwasema, ‘Mtu akiapa kwa Hekalu, kiapo hicho si kitu; lakini mtu akiapa kwa dhahabu ya Hekalu, amefungwa kwa kiapo chake.’ 17Ninyi vipofu wapumbavu! Ni kipi kilicho kikuu zaidi: ni ile dhahabu, au ni lile Hekalu linaloifanya hiyo dhahabu kuwa takatifu? 18Pia mnasema, ‘Mtu akiapa kwa madhabahu, si kitu; lakini mtu akiapa kwa sadaka iliyo juu ya madhabahu, amefungwa kwa kiapo chake’ 19Ninyi vipofu! Ni kipi kikuu zaidi: ni sadaka, au ni madhabahu yanayoifanya hiyo sadaka kuwa takatifu? 20Basi, mtu anayeapa kwa madhabahu, anaapa kwa hayo madhabahu na vitu vyote vilivyo juu yake. 21Naye mtu anayeapa kwa Hekalu, anaapa kwa hilo Hekalu na kwa huyo akaaye ndani yake. 22Naye anayeapa kwa mbingu, anaapa kwa kiti cha enzi cha Mungu na kwa yeye anayeketi kwenye kiti hicho.
23“Ole wenu walimu wa Torati na Mafarisayo, ninyi wanafiki! Kwa maana mnatoa zaka ya mnanaa, bizari na jira, lakini mmeacha mambo makuu zaidi ya sheria, yaani haki, huruma na uaminifu. Iliwapasa kufanya haya makuu ya sheria bila kupuuza hayo matoleo. 24Ninyi viongozi vipofu, mnachuja kiroboto lakini mnameza ngamia!
25“Ole wenu, walimu wa Torati na Mafarisayo, ninyi wanafiki! Kwa maana mnasafisha kikombe na sahani kwa nje, lakini ndani mmejaa unyang’anyi na kutokuwa na kiasi. 26Ewe Farisayo kipofu! Safisha ndani ya kikombe na sahani kwanza, ndipo nje itakuwa safi pia.
27“Ole wenu, walimu wa Torati na Mafarisayo, ninyi wanafiki! Mnafanana na makaburi yaliyopakwa chokaa, ambayo yanapendeza kwa nje, lakini ndani yamejaa mifupa ya wafu na kila aina ya uchafu. 28Vivyo hivyo, kwa nje ninyi mnaonekana kwa watu kuwa wenye haki, lakini kwa ndani mmejaa unafiki na uovu.
29“Ole wenu, walimu wa Torati na Mafarisayo, ninyi wanafiki! Mnajenga makaburi ya manabii na kuyapamba makaburi ya wenye haki. 30Nanyi mwasema, ‘Kama tungeishi wakati wa baba zetu, hatungeshiriki katika kumwaga damu ya manabii!’ 31Hivyo mnajishuhudia wenyewe kwamba ninyi ni wana wa wale waliowaua manabii. 32Haya basi, kijazeni kipimo cha dhambi ya baba zenu!
33“Ninyi nyoka, ninyi uzao wa nyoka wenye sumu! Mtaiepukaje hukumu ya Jehanamu? 34Kwa sababu hii, tazameni, natuma kwenu manabii na wenye hekima na walimu. Baadhi yao mtawaua na kuwasulubisha, na wengine wao mtawapiga mijeledi katika masinagogi yenu na kuwafuatia kutoka mji mmoja hadi mji mwingine. 35Hivyo ile damu ya wenye haki wote iliyomwagwa hapa duniani, tangu damu ya Habili, aliyekuwa mwenye haki, hadi damu ya Zakaria mwana wa Barakia, mliyemuua kati ya patakatifu na madhabahu, itawajia juu yenu. 36Amin, nawaambia, haya yote yatakuja kwa kizazi hiki.
Isa aomboleza kwa ajili ya Yerusalemu
(Luka 13:34-35)
37“Ee Yerusalemu, Yerusalemu, uwauaye manabii na kuwapiga mawe wale waliotumwa kwako! Mara ngapi nimetamani kuwakusanya watoto wako pamoja, kama vile kuku akusanyavyo vifaranga wake chini ya mabawa yake, lakini hukutaka! 38Tazama nyumba yenu imeachwa ukiwa. 39Kwa maana nawaambia, hamtaniona tena tangu sasa hadi mtakaposema, ‘Amebarikiwa yeye ajaye kwa Jina la Mwenyezi Mungu.’#23:39 Zaburi 118:26”
Iliyochaguliwa sasa
Mathayo 23: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapistaging.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.