Mathayo 24:42-51
Mathayo 24:42-51 NEN
“Basi kesheni, kwa sababu hamjui ni siku gani atakapokuja Bwana wenu. Lakini fahamuni jambo hili: Kama mwenye nyumba angejua ni wakati gani wa usiku ambao mwizi atakuja, angekesha na hangekubali nyumba yake kuvunjwa. Kwa hiyo ninyi pia hamna budi kuwa tayari, kwa sababu Mwana wa Adamu atakuja saa msiyotazamia. “Ni nani basi aliye mtumishi mwaminifu na mwenye busara, ambaye bwana wake amemweka kusimamia watumishi wengine katika nyumba yake, ili awape chakula chao kwa wakati unaofaa? Heri mtumishi yule ambaye bwana wake atakaporudi atamkuta akifanya hivyo. Amin, nawaambia, atamweka mtumishi huyo kuwa msimamizi wa mali yake yote. Lakini kama huyo mtumishi ni mwovu, naye akasema moyoni mwake, ‘Bwana wangu atakawia muda mrefu,’ kisha akaanza kuwapiga watumishi wenzake, na kula na kunywa pamoja na walevi. Basi bwana wa mtumishi huyo atakuja siku asiyodhani na saa asiyoijua. Atamkata vipande vipande na kumweka katika sehemu moja pamoja na wanafiki, mahali ambako kutakuwa ni kulia na kusaga meno.