Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 27:11-26

Mathayo 27:11-26 NEN

Wakati huo Yesu akiwa amesimama mbele ya mtawala, mtawala akamuuliza, “Wewe ndiye mfalme wa Wayahudi?” Yesu akasema, “Wewe wasema hivyo.” Lakini viongozi wa makuhani na wazee walipomshtaki, hakujibu neno. Ndipo Pilato akamuuliza, “Je, husikii ni mambo mangapi wanayokushtaki nayo?” Lakini Yesu hakumjibu hata kwa shtaka moja, kiasi kwamba mtawala alishangaa sana. Basi ilikuwa ni desturi ya mtawala kumfungua mfungwa mmoja aliyechaguliwa na umati wa watu wakati wa sikukuu. Wakati huo alikuwepo mfungwa mmoja mwenye sifa mbaya, aliyeitwa Baraba. Hivyo umati wa watu walipokusanyika, Pilato akawauliza, “Mnataka niwafungulie nani, Baraba au Yesu yeye aitwaye Kristo?” Kwa kuwa alitambua Yesu alikuwa amekabidhiwa kwake kwa ajili ya wivu. Pilato akiwa ameketi kwenye kiti cha hukumu, mkewe akampelekea ujumbe huu: “Usiwe na jambo lolote juu ya mtu huyu asiye na hatia, kwa kuwa leo nimeteseka sana katika ndoto kwa sababu yake.” Lakini viongozi wa makuhani na wazee wakaushawishi ule umati wa watu kwamba waombe Baraba afunguliwe, naye Yesu auawe. Mtawala akawauliza tena, “Ni yupi kati ya hawa wawili mnayetaka niwafungulie?” Wakajibu, “Baraba.” Pilato akawaambia, “Basi nifanye nini na huyu Yesu aitwaye Kristo?” Wakajibu wote, “Msulubishe!” Pilato akauliza, “Kwa nini? Amefanya kosa gani?” Lakini wao wakazidi kupiga kelele, wakisema, “Msulubishe!” Pilato alipoona kwamba hawezi kufanya lolote, lakini badala yake ghasia zilikuwa zinaanza, akachukua maji, akanawa mikono yake mbele ya ule umati wa watu, akasema, “Sina hatia juu ya damu ya mtu huyu, hili ni jukumu lenu!” Watu wote wakajibu, “Damu yake na iwe juu yetu na juu ya watoto wetu!” Basi akawafungulia Baraba. Lakini baada ya kuamuru Yesu achapwe mijeledi, akamtoa ili asulubishwe.

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Mathayo 27:11-26