Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 28

28
Isa afufuka
(Marko 16:1-10; Luka 24:1-12; Yohana 20:1-10)
1Baada ya Sabato, alfajiri mapema siku ya kwanza ya juma, Mariamu Magdalene na yule Mariamu mwingine walienda kulitazama kaburi.
2Ghafula, pakawa na tetemeko kubwa la ardhi, kwa sababu malaika wa Mwenyezi Mungu alishuka kutoka mbinguni, akaenda kwenye kaburi, akalivingirisha lile jiwe na kulikalia. 3Sura ya huyo malaika ilikuwa kama umeme, na mavazi yake yalikuwa meupe kama theluji. 4Wale walinzi wa kaburi walimwogopa sana, wakatetemeka hata wakawa kama wafu.
5Yule malaika akawaambia wale wanawake, “Msiogope, kwa maana ninajua kuwa mnamtafuta Isa aliyesulubiwa. 6Hayupo hapa, kwa kuwa amefufuka, kama alivyosema. Njooni mpatazame mahali alipokuwa amelazwa. 7Kisha nendeni upesi mkawaambie wanafunzi wake kwamba, ‘Amefufuka kutoka kwa wafu, naye anawatangulia kwenda Galilaya. Mtamwona huko.’ Sasa nimekwisha kuwaambia.”
8Hivyo wale wanawake wakaondoka pale kaburini wakiwa wamejawa na hofu, lakini wakiwa na furaha nyingi. Wakaenda mbio kuwaeleza wanafunzi wake habari hizo. 9Ghafula, Isa akakutana nao, akasema, “Salamu!” Wale wanawake wakamkaribia, wakaishika miguu yake, wakamwabudu. 10Ndipo Isa akawaambia, “Msiogope. Nendeni mkawaambie ndugu zangu waende Galilaya, ndiko watakakoniona.”
Taarifa ya walinzi
11Wale wanawake wakiwa njiani wakienda, baadhi ya wale askari waliokuwa wakilinda kaburi walienda mjini na kuwaeleza viongozi wa makuhani kila kitu kilichokuwa kimetukia. 12Baada ya viongozi wa makuhani kukutana na wazee na kupanga njama, waliwapa wale askari kiasi kikubwa cha fedha, 13wakawaambia, “Semeni, ‘Wanafunzi wake walikuja wakati wa usiku na kumwiba sisi tulipokuwa tumelala.’ 14Kama habari hizi zikimfikia mtawala, sisi tutamwondolea mashaka nanyi hamtapata tatizo lolote.” 15Hivyo basi, wale askari wakazipokea hizo fedha nao wakafanya kama walivyoelekezwa. Habari hii imeenea miongoni mwa Wayahudi hadi leo.
Isa awatuma wanafunzi wake
(Marko 16:14-18; Luka 24:36-49; Yohana 20:19-23; Matendo 1:6-8)
16Basi wale wanafunzi kumi na mmoja wakaenda hadi Galilaya kwenye ule mlima ambao Isa alikuwa amewaagiza. 17Walipomwona, wakamwabudu; lakini baadhi yao wakaona shaka. 18Isa akawajia na kusema, “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. 19Kwa sababu hii, nendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza#28:19 Ubatizo ni ishara ya kuungama dhambi na kusamehewa na Mwenyezi Mungu, na kuweka nadhiri ya kubadilisha mienendo ya awali. kwa Jina la Baba#28:19 Jina Baba linaonesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu. na la Mwana#28:19 Yaani Isa Al-Masihi, aliye na asili ya Mwenyezi Mungu, na uhusiano wa kipekee naye. na la Roho#28:19 Ndiye anayefanya kazi ya Mwenyezi Mungu katika moyo wa mwanadamu, na kumshawishi nia yake kumfuata Isa Al-Masihi (Yohana 16:5-15). wa Mungu, 20nanyi wafundisheni kuyashika mambo yote niliyowaamuru ninyi. Hakika mimi niko pamoja nanyi siku zote, hadi mwisho wa nyakati.”

Iliyochaguliwa sasa

Mathayo 28: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia