Mathayo 7
7
Kuwahukumu wengine
(Luka 6:37-38, 41-42)
1“Usihukumu ili usije ukahukumiwa. 2Kwa maana jinsi unavyowahukumu wengine, ndivyo utakavyohukumiwa, na kwa kipimo kile upimiacho, ndicho utakachopimiwa.
3“Mbona unatazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako, na wala huoni boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe? 4Au unawezaje kumwambia ndugu yako, ‘Acha nitoe kibanzi kwenye jicho lako,’ wakati kuna boriti kwenye jicho lako mwenyewe? 5Ewe mnafiki, ondoa boriti ndani ya jicho lako kwanza, ndipo utaweza kuona dhahiri jinsi ya kuondoa kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako.
6“Msiwape mbwa vitu vilivyo vitakatifu; wala msitupie nguruwe lulu zenu. Mkifanya hivyo, watazikanyagakanyaga na kisha watawageukia na kuwararua vipande vipande.
Omba, tafuta, bisha
(Luka 11:9-13)
7“Ombeni nanyi mtapewa; tafuteni nanyi mtapata; bisheni nanyi mtafunguliwa mlango. 8Kwa kuwa kila aombaye hupewa; naye kila atafutaye hupata; na kila abishaye hufunguliwa mlango.
9“Au ni nani miongoni mwenu ambaye mwanawe akimwomba mkate atampa jiwe? 10Au mwanawe akimwomba samaki atampa nyoka? 11Basi ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vitu vizuri, si zaidi sana Baba#7:11 Jina Baba linaonesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu. Kwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu ni Baba kupitia uhusiano unaopatikana katika kumtumaini Isa Al-Masihi. yenu aliye mbinguni atawapa vitu vizuri wale wamwombao? 12Kwa hiyo chochote mnachotaka mtendewe na watu, ninyi nanyi watendeeni vivyo hivyo. Kwa kuwa hii ndiyo Torati na Manabii.
Mlango mwembamba na njia pana
13“Ingieni kupitia mlango mwembamba, kwa maana lango ni pana na njia ni pana ielekeayo upotevuni, nao ni wengi wanaoingia kupitia lango hilo. 14Lakini mlango ni mwembamba na njia ni finyu ielekeayo kwenye uzima, nao ni wachache tu waionao.
Mti na matunda yake
(Marko 12:33-35; Luka 6:43-44)
15“Jihadharini na manabii wa uongo, wanaowajia wakiwa wamevaa mavazi ya kondoo, lakini ndani ni mbwa-mwitu wakali. 16Mtawatambua kwa matunda yao. Je, watu huchuma zabibu kwenye miiba, au tini kwenye michongoma? 17Vivyo hivyo, mti mwema huzaa matunda mazuri, na mti mbaya huzaa matunda mabaya. 18Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mbaya hauwezi kuzaa matunda mazuri. 19Kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni. 20Hivyo, mtawatambua kwa matunda yao.
Mwanafunzi wa kweli
(Luka 13:25-27)
21“Si kila mtu aniambiaye, ‘Bwana, Bwana,’ atakayeingia katika ufalme wa mbinguni, bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni. 22Wengi wataniambia siku ile, ‘Bwana, Bwana, hatukutoa unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo wachafu na kufanya miujiza mingi?’ 23Ndipo nitakapowaambia wazi, ‘Sikuwajua kamwe. Ondokeni kwangu, ninyi watenda maovu!’
Mjenzi mwenye busara na mjenzi mpumbavu
(Luka 6:47-49)
24“Kwa hiyo kila mtu ayasikiaye haya maneno yangu na kuyatenda, ni kama mtu mwenye busara aliyejenga nyumba yake kwenye mwamba. 25Mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, na upepo ukavuma ukaipiga hiyo nyumba. Lakini haikuanguka; kwa sababu msingi wake ulikuwa kwenye mwamba. 26Kila anayesikia haya maneno yangu na asiyatende ni kama mtu mjinga aliyejenga nyumba yake kwenye mchanga. 27Mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, nao upepo ukavuma ukaipiga hiyo nyumba, nayo ikaanguka kwa kishindo kikubwa.”
28Isa alipomaliza kusema maneno haya, umati wa watu wakashangazwa sana na mafundisho yake, 29kwa sababu alifundisha kama yeye aliye na mamlaka, wala si kama walimu wao wa sheria.
Iliyochaguliwa sasa
Mathayo 7: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.