Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 8:1-13

Mathayo 8:1-13 NENO

Isa aliposhuka kutoka mlimani, makundi ya watu wakamfuata. Mtu mmoja mwenye ukoma akaja na kupiga magoti mbele yake, akasema, “Bwana, ukitaka, unaweza kunitakasa.” Isa akanyoosha mkono wake akamgusa yule mtu, akamwambia, “Nataka. Takasika!” Mara yule mtu akatakasika ukoma wake. Kisha Isa akamwambia, “Hakikisha humwambii mtu yeyote. Lakini nenda ukajioneshe kwa kuhani, na utoe sadaka aliyoamuru Musa, ili kuwa ushuhuda kwao.” Isa alipoingia Kapernaumu, jemadari mmoja alimjia, kumwomba msaada, akisema, “Bwana, mtumishi wangu amelala nyumbani na amepooza, tena ana maumivu makali ya kutisha.” Isa akamwambia, “Nitakuja na kumponya.” Lakini yule jemadari akamwambia, “Bwana, mimi sistahili wewe kuingia ndani ya nyumba yangu. Lakini sema neno tu, naye mtumishi wangu atapona. Kwa kuwa mimi mwenyewe ni mtu niliye chini ya mamlaka, nikiwa na askari chini yangu. Nikimwambia huyu, ‘Nenda,’ yeye huenda; na mwingine nikimwambia, ‘Njoo,’ yeye huja. Nikimwambia mtumishi wangu, ‘Fanya hivi,’ yeye hufanya.” Isa aliposikia maneno haya, alishangaa, akawaambia wale waliomfuata, “Amin, nawaambia, hata katika Israeli sijapata kuona yeyote mwenye imani kubwa namna hii. Ninawaambia kwamba wengi watatoka mashariki na magharibi, nao wataketi karamuni pamoja na Ibrahimu, Isaka na Yakobo katika ufalme wa mbinguni. Lakini warithi wa ufalme watatupwa katika giza la nje, ambako kutakuwa kilio na kusaga meno.” Kisha Isa akamwambia yule jemadari, “Nenda na iwe kwako sawasawa na imani yako.” Naye yule mtumishi akapona wakati ule ule.