Mt 8:1-13
Mt 8:1-13 SUV
Naye aliposhuka mlimani, makutano mengi walimfuata. Na tazama, akaja mtu mwenye ukoma akamsujudia, akisema, Bwana, ukitaka, waweza kunitakasa. Yesu akanyosha mkono, akamgusa, akisema Nataka; takasika. Na mara ukoma wake ukatakasika. Yesu akamwambia, Angalia, usimwambie mtu; ila enenda zako, ukajionyeshe kwa kuhani, ukaitoe sadaka kama alivyoamuru Musa, iwe ushuhuda kwao. Hata alipoingia Kapernaumu, akida mmoja alimjia, akamsihi, akisema, Bwana, mtumishi wangu amelala nyumbani, mgonjwa wa kupooza, anaumwa sana. Yesu akamwambia, Nitakuja, nimponye. Yule akida akamjibu, akasema, Bwana, mimi sistahili wewe uingie chini ya dari yangu; lakini sema neno tu, na mtumishi wangu atapona. Kwa maana mimi nami ni mtu niliyewekwa chini ya mamlaka, mwenye askari chini yangu; nikimwambia huyu, Nenda, huenda; na huyu, Njoo, huja; na mtumwa wangu, Fanya hivi, hufanya. Yesu aliposikia hayo, alistaajabu, akawaambia wale waliomfuata, Amin, nawaambieni, Sijaona imani kubwa namna hii, kwa ye yote katika Israeli. Nami nawaambieni, ya kwamba wengi watakuja kutoka mashariki na magharibi, nao wataketi pamoja na Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo katika ufalme wa mbinguni; bali wana wa ufalme watatupwa katika giza la nje, ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. Naye Yesu akamwambia yule akida, Nenda zako; na iwe kwako kama ulivyoamini. Mtumishi wake akapona saa ile ile.