Mathayo 8:14-22
Mathayo 8:14-22 NENO
Isa alipoingia nyumbani mwa Petro, alimkuta mama mkwe wa Petro amelala kitandani, akiwa ana homa. Akamgusa mkono wake na homa ikamwacha, naye akainuka na kuanza kumhudumia. Jioni ile, wakamletea watu wengi waliopagawa na pepo wachafu, naye akawatoa wale pepo wachafu kwa neno lake, na kuwaponya wagonjwa wote. Haya yalifanyika ili litimie neno lililonenwa kwa kinywa cha nabii Isaya, kwamba: “Mwenyewe alitwaa udhaifu wetu na akachukua magonjwa yetu.” Isa alipoona makundi mengi yamemzunguka, aliwaamuru wanafunzi wake wavuke hadi ng’ambo ya ziwa. Kisha mwalimu mmoja wa sheria akamjia Isa na kumwambia, “Mwalimu, nitakufuata popote utakakoenda.” Naye Isa akamjibu, “Mbweha wana mapango, nao ndege wa angani wana viota, lakini Mwana wa Adamu hana mahali pa kulaza kichwa chake.” Mwanafunzi mwingine akamwambia, “Bwana, niruhusu kwanza nikamzike baba yangu.” Lakini Isa akamwambia, “Nifuate, uwaache wafu wawazike wafu wao.”