Marko 12
12
Mfano wa wapangaji waovu
(Mathayo 21:33-46; Luka 20:9-19)
1Isa akaanza kusema nao kwa mifano, akawaambia: “Mtu mmoja alipanda shamba la mizabibu. Akajenga ukuta kulizunguka, na ndani yake akachimba shimo la shinikizo la kukamulia zabibu, na akajenga mnara wa ulinzi. Kisha akalikodisha shamba hilo la mizabibu kwa wakulima fulani, kisha akasafiri hadi nchi nyingine. 2Wakati wa mavuno ulipofika, mwenye shamba akamtuma mtumishi wake kwa hao wapangaji ili kuchukua sehemu yake ya mavuno ya shamba la mizabibu kutoka kwa hao wapangaji. 3Lakini wale wakulima walimkamata yule mtumishi, wakampiga, wakamfukuza mikono mitupu. 4Kisha yule mwenye shamba akamtuma mtumishi mwingine kwao; nao wale wakulima wakampiga kichwani na kumfanyia mambo ya aibu. 5Kisha akamtuma mtumishi mwingine, naye huyo wakamuua. Akawatuma wengine wengi; baadhi yao wakawapiga, na wengine wakawaua.
6“Mwenye shamba alikuwa bado na mmoja wa kumtuma, mwanawe aliyempenda. Hatimaye akamtuma akisema, ‘Watamheshimu mwanangu.’
7“Lakini wale wapangaji wakasemezana pamoja, ‘Huyu ndiye mrithi. Njooni tumuue, nao urithi utakuwa wetu.’ 8Hivyo wakamchukua na kumuua, wakamtupa nje ya lile shamba la mizabibu.
9“Sasa basi yule mwenye shamba atafanya nini? Atakuja na kuwaua hao wapangaji, kisha atawapa wapangaji wengine hilo shamba la mizabibu. 10Je, hamjasoma andiko hili:
“ ‘Jiwe walilolikataa waashi
limekuwa jiwe kuu la pembeni;
11Mwenyezi Mungu ndiye alitenda jambo hili,
nalo ni la kushangaza machoni petu’#12:11 Zaburi 118:22, 23?”
12Walipotambua kuwa amesema mfano huo kwa ajili yao, wakataka kumkamata, lakini wakaogopa umati ule wa watu. Wakamwacha, wakaenda zao.
Swali kuhusu kulipa kodi ya Kaisari
(Mathayo 22:15-22; Luka 20:20-26)
13Baadaye wakawatuma baadhi ya Mafarisayo#12:13 Kundi la kidini la Wayahudi; walifuata Torati kwa dhati, hasa maagizo kuhusu utakaso. Pia waliamini katika malaika, ufufuo wa wafu, na kuja kwa Masihi ambaye atarejesha ufalme wa Daudi na ukuu wa taifa la Israeli. na Maherode#12:13 Wafuasi wa Mfalme Herode waliokubaliana na utawala wa Rumi. ili wamtege Isa katika maneno yake. 14Wakamjia, wakamwambia, “Mwalimu, tunajua kwamba wewe ni mtu mwadilifu. Wewe huyumbishwi na wanadamu, kwa kuwa huna upendeleo. Lakini wewe huifundisha njia ya Mungu katika kweli. Je, ni halali kulipa kodi kwa Kaisari, au la? 15Je, tulipe kodi au tusilipe?”
Lakini Isa alijua unafiki wao. Akawauliza, “Mbona mnajaribu kunitega? Nileteeni hiyo dinari#12:15 dinari moja ilikuwa sawa na mshahara wa kibarua wa siku moja. niione.” 16Wakamletea hiyo sarafu. Naye akawauliza, “Sura hii ni ya nani? Na maandishi haya ni ya nani?”
Wakamjibu, “Ni vya Kaisari.”
17Ndipo Isa akawaambia, “Mpeni Kaisari kilicho cha Kaisari, naye Mungu mpeni kilicho cha Mungu.”
Nao wakamstaajabia sana.
Ndoa wakati wa ufufuo
(Mathayo 22:23-33; Luka 20:27-40)
18Kisha Masadukayo, wale wasemao kuwa hakuna ufufuo wa wafu, wakamjia Isa, 19wakasema, “Mwalimu, Musa alituandikia kuwa kama ndugu wa mtu akifa na kumwacha mkewe bila mtoto, basi huyo mtu inampasa amwoe huyo mjane ili amzalie ndugu yake watoto. 20Basi kulikuwa na ndugu saba. Yule wa kwanza akaoa mke, naye akafa bila kuacha mtoto yeyote. 21Wa pili akamwoa yule mjane, lakini naye akafa bila kuacha mtoto yeyote. Ikawa vivyo hivyo kwa yule wa tatu. 22Hakuna hata mmoja wa hao ndugu saba aliyeacha mtoto. Hatimaye yule mwanamke naye akafa. 23Basi, wakati wa ufufuo yeye atakuwa mke wa nani, maana aliolewa na ndugu wote saba?”
24Isa akawajibu, “Je, hampotei kwa sababu hamfahamu Maandiko wala uweza wa Mungu? 25Wafu watakapofufuka, hawataoa wala kuolewa, bali watakuwa kama malaika wa mbinguni. 26Basi kuhusu wafu kufufuliwa, je hamjasoma katika Kitabu cha Musa jinsi Mungu alivyosema na Musa kutoka kile kichaka akisema, ‘Mimi ni Mungu wa Ibrahimu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo’#12:26 Kutoka 3:6? 27Yeye si Mungu wa wafu, bali ni Mungu wa walio hai. Kwa hiyo mmekosea kabisa.”
Amri kuu kuliko zote
(Mathayo 22:34-40; Luka 10:25-28)
28Mwalimu mmoja wa sheria akaja, akawasikia wakijadiliana. Akiona kwamba Isa amewajibu vyema, naye akamuuliza, “Katika amri zote, ni ipi iliyo kuu?”
29Isa akajibu, “Amri iliyo kuu ndiyo hii: ‘Sikia ee Israeli. Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, Bwana ndiye mmoja. 30Mpende Mwenyezi Mungu, Mungu wako, kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote.’#12:30 Kumbukumbu 6:4, 5 31Ya pili ndiyo hii: ‘Mpende jirani yako kama nafsi yako.’#12:31 Walawi 19:18 Hakuna amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi.”
32Yule mwalimu wa Torati akamwambia Isa, “Mwalimu, umejibu vyema kwamba Mungu ni mmoja, wala hakuna mwingine ila yeye. 33Kumpenda Mungu kwa moyo wako wote, na kwa ufahamu wako wote, na kwa nguvu zako zote, na kumpenda jirani kama mtu anavyojipenda mwenyewe ni bora kuliko kutoa sadaka za kuteketezwa na dhabihu zote.”
34Isa alipoona kwamba amejibu kwa busara, akamwambia, “Wewe huko mbali na ufalme wa Mungu.” Tangu wakati huo, hakuna mtu yeyote aliyethubutu kumuuliza maswali tena.
Al-Masihi ni Mwana wa nani?
(Mathayo 22:41-46; Luka 20:41-44)
35Isa alipokuwa akifundisha Hekaluni, akauliza, “Imekuwaje walimu wa Torati wanasema kwamba Al-Masihi#12:35 Al-Masihi maana yake Aliyetiwa mafuta. ni Mwana wa Daudi? 36Kwa maana Daudi mwenyewe, akinena kwa kuongozwa na Roho wa Mungu, alisema:
“ ‘Bwana alimwambia Bwana wangu:
“Keti mkono wangu wa kuume,
hadi nitakapowaweka adui zako
chini ya miguu yako.”#12:36 Zaburi 110:1’
37Kwa hiyo Daudi mwenyewe anamwita ‘Bwana.’ Awezaje basi yeye kuwa mwanawe?”
Umati ule wote wa watu wakamsikiliza kwa furaha.
Isa atahadharisha kuhusu walimu wa Torati
(Mathayo 23:1-36; Luka 20:45-47)
38Alipokuwa akifundisha, Isa alisema, “Jihadharini na walimu wa Torati. Wao hupenda kutembea wakiwa wamevaa mavazi marefu, na kusalimiwa kwa heshima masokoni. 39Pia wao hupenda kukaa kwenye viti vya mbele katika masinagogi#12:39 Nyumba za ibada na mafunzo., na kupewa nafasi za heshima katika karamu. 40Wao hula nyumba za wajane, na ili waonekane kuwa wema wanasali sala ndefu. Watu kama hawa watapata hukumu iliyo kuu sana.”
Sadaka ya mjane maskini
(Luka 21:1-4)
41Kisha Isa akaketi mkabala na sehemu ambapo sadaka zilikuwa zinawekwa na kuangalia umati wa watu wakiweka fedha zao kwenye sanduku la hazina ya Hekalu. Matajiri wengi wakaweka kiasi kikubwa cha fedha. 42Lakini mjane mmoja maskini akaja na kuweka sarafu mbili ndogo za shaba zenye thamani ya senti mbili.
43Isa akawaita wanafunzi wake, akawaambia, “Amin, nawaambia, huyu mjane maskini ameweka katika sanduku la hazina zaidi ya watu wengine wote. 44Wengine wote wametoa kutokana na ziada ya mali yao. Lakini huyu mjane ametoa kutokana na umaskini wake, akaweka kila kitu alichokuwa nacho, hata kile alichohitaji ili kuishi.”
Iliyochaguliwa sasa
Marko 12: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapistaging.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.