Marko 13:28-37
Marko 13:28-37 NEN
“Basi jifunzeni somo hili kutokana na mtini: Matawi yake yanapoanza kuchipua na kutoa majani, mnatambua kwamba wakati wa kiangazi umekaribia. Vivyo hivyo, myaonapo mambo haya yakitukia, mnatambua kwamba wakati u karibu, hata malangoni. Amin, nawaambia, kizazi hiki hakitapita hadi mambo haya yote yawe yametimia. Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe. “Kwa habari ya siku ile na saa hakuna yeyote ajuaye, hata malaika walio mbinguni wala Mwana, ila Baba peke yake. Jihadharini! Kesheni! Kwa maana hamjui wakati ule utakapowadia. Ni kama mtu anayesafiri. Anaiacha nyumba yake na kuwaachia watumishi wake kuiangalia, kila mtu na kazi yake, kisha akamwamuru yule bawabu aliye mlangoni akeshe. “Basi kesheni kwa sababu hamjui ni lini mwenye nyumba atakaporudi: iwapo ni jioni, au ni usiku wa manane, au alfajiri awikapo jogoo, au mapambazuko. Kama akija ghafula, asije akawakuta mmelala. Lile ninalowaambia ninyi, nawaambia watu wote: ‘Kesheni!’ ”