Marko 13:28-37
Marko 13:28-37 SRUV
Kwa mtini jifunzeni mfano; tawi lake liishapo kuwa laini, na kuchanua majani, mwatambua ya kuwa wakati wa mavuno ni karibu; nanyi kadhalika, myaonapo mambo hayo yanaanza, tambueni ya kuwa yu karibu milangoni. Amin, nawaambieni, Kizazi hiki hakitapita, hata hayo yote yatimie. Mbingu na nchi zitapita; lakini maneno yangu hayatapita kamwe. Lakini habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana, ila Baba. Angalieni, kesheni, [ombeni], kwa kuwa hamjui wakati ule utakapokuwapo. Mfano wake ni kama mtu mwenye kusafiri, ameiacha nyumba yake, amewapa watumwa wake amri, na kila mtu kazi yake, naye amemwamuru bawabu akeshe. Kesheni basi, kwa maana hamjui ajapo bwana wa nyumba, kwamba ni jioni, au kwamba ni usiku wa manane, au awikapo jogoo, au asubuhi; asije akawasili ghafla akawakuta mmelala. Na hilo niwaambialo ninyi, nawaambia wote, Kesheni.