1
Salamu
1Paulo na Timotheo, watumishi wa Al-Masihi Isa.
Kwa watakatifu wote katika Al-Masihi Isa walio Filipi, pamoja na waangalizi na mashemasi.
2Neema na amani zinazotoka kwa Mungu, Baba#1:2 Kwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu ni Baba kupitia uhusiano unaopatikana katika kumtumaini Isa Al-Masihi. yetu, na kwa Bwana wetu Isa Al-Masihi ziwe nanyi.
Shukrani na maombi
3Ninamshukuru Mungu wangu kila niwakumbukapo ninyi. 4Katika maombi yangu yote daima nimekuwa nikiwaombea ninyi nyote kwa furaha, 5kwa sababu ya kushiriki kwenu katika kueneza Injili, tangu siku ya kwanza hadi leo. 6Nina hakika kwamba yeye aliyeianza kazi njema mioyoni mwenu, ataiendeleza na kuikamilisha hata siku ya Al-Masihi Isa.
7Ni haki na ni wajibu wangu kufikiri hivi juu yenu nyote, kwa sababu ninyi mko moyoni mwangu. Ikiwa nimefungwa au nikiwa ninaitetea na kuithibitisha Injili, ninyi nyote mnashiriki neema ya Mungu pamoja nami. 8Mungu ni shahidi wangu jinsi ninavyowaonea shauku ninyi nyote kwa huruma ya Al-Masihi Isa.
9Haya ndio maombi yangu: kwamba upendo wenu uongezeke zaidi na zaidi katika maarifa na ufahamu wote, 10ili mpate kutambua yale yaliyo mema, mkawe safi, wasio na hatia hadi siku ya Al-Masihi, 11mkiwa mmejawa na matunda ya haki yapatikanayo kupitia kwa Isa Al-Masihi, kwa utukufu na sifa za Mungu.
Kufungwa kwa Paulo kwaieneza Injili
12Basi, ndugu zangu, nataka mjue kwamba mambo yale yaliyonipata kwa kweli yamesaidia sana kueneza Injili. 13Matokeo yake ni kwamba imejulikana wazi kwa walinzi wote wa jumba la kifalme na kwa wengine wote kuwa nimefungwa kwa ajili ya Al-Masihi. 14Kwa sababu ya vifungo vyangu, ndugu wengi katika Bwana Isa wametiwa moyo kuhubiri neno la Mungu kwa ujasiri zaidi na bila woga.
15Ni kweli kwamba wengine wanamhubiri Al-Masihi kutokana na wivu na kwa kutaka kushindana, lakini wengine wanamhubiri Al-Masihi kwa nia njema. 16Hawa wa mwisho wanamhubiri Al-Masihi kwa moyo wa upendo, wakifahamu kwamba nimo humu gerezani kwa ajili ya kuitetea Injili. 17Hao wa kwanza wanamtangaza Al-Masihi kutokana na tamaa zao wenyewe wala si kwa moyo mweupe, bali wanakusudia kuongeza mateso yangu katika huku kufungwa kwangu. 18Lakini inadhuru nini? Jambo la muhimu ni kwamba kwa kila njia, ikiwa ni kwa nia mbaya au njema, Al-Masihi anahubiriwa. Nami kwa ajili ya jambo hilo ninafurahi.
Naam, nami nitaendelea kufurahi, 19kwa maana ninajua kwamba kwa maombi yenu na kwa msaada unaotolewa na Roho wa Isa Al-Masihi, yale yaliyonipata mimi yatageuka kuwa wokovu wangu. 20Ninatarajia kwa shauku kubwa na kutumaini kwamba sitaaibika kwa njia yoyote, bali nitakuwa na ujasiri wa kutosha ili sasa kama wakati mwingine wowote, Al-Masihi atukuzwe katika mwili wangu, ikiwa ni kwa kuishi au kwa kufa. 21Kwa maana kwangu mimi, kuishi ni Al-Masihi, na kufa ni faida. 22Kama nitaendelea kuishi katika mwili, kwangu hili ni kwa ajili ya matunda ya kazi. Lakini nichague lipi? Mimi sijui! 23Ninavutwa kati ya mambo mawili: Ninatamani kuondoka nikakae pamoja na Al-Masihi, jambo hilo ni bora zaidi. 24Lakini kwa sababu yenu ni muhimu zaidi mimi nikiendelea kuishi katika mwili. 25Nikiwa na hakika ya jambo hili, ninajua kwamba nitaendelea kuwepo pamoja nanyi nyote, ili mpate kukua na kuwa na furaha katika imani, 26ili kwa kuja kwangu kwenu tena, furaha yenu iwe nyingi katika Al-Masihi Isa kwa ajili yangu.
Kuenenda ipasavyo Injili
27Lakini lolote litakalotukia, mwenende kama ipasavyo Injili ya Al-Masihi, ili nikija na kuwaona au ikiwa sipo, nipate kusikia haya juu yenu: Kuwa mnasimama imara katika roho moja, mkiishindania imani ya Injili kwa umoja, 28wala msitishwe na wale wanaowapinga. Hii ni ishara kwao kuwa wataangamia, lakini ninyi mtaokolewa, na hii ni kazi ya Mungu. 29Kwa maana mmepewa kwa ajili ya Al-Masihi, si kumwamini tu, bali pia kuteswa kwa ajili yake, 30kwa kuwa mnashiriki mashindano yale yale mliyoyaona nikiwa nayo na ambayo hata sasa mnasikia kuwa bado ninayo.