2
Kuiga unyenyekevu wa Al-Masihi
1Kama kukiwa na jambo lolote la kutia moyo katika kuunganishwa na Al-Masihi, kukiwa faraja yoyote katika upendo wake, kukiwa na ushirika wowote na Roho wa Mungu, kukiwa na wema wowote na huruma, 2basi ikamilisheni furaha yangu kwa kuwa na nia moja, mkiwa na upendo huo moja, mkiwa wa roho na kusudi moja. 3Msitende jambo lolote kwa nia ya kujitukuza wala kujivuna, bali kwa unyenyekevu kila mtu amhesabu mwingine bora kuliko nafsi yake. 4Kila mmoja wenu asiangalie faida yake mwenyewe tu, bali pia ajishughulishe kwa faida ya wengine.
5Kuweni na nia ile ile aliyokuwa nayo Al-Masihi Isa:
6Yeye, ingawa alikuwa na asili ya Mungu hasa,
hakuona kule kuwa sawa na Mungu
kuwa kitu cha kushikilia,
7bali alijifanya si kitu,
akachukua hali hasa ya mtumwa,
naye akazaliwa katika umbo la mwanadamu.
8Naye akiwa na umbo la mwanadamu,
alijinyenyekeza, akatii hata mauti:
naam, mauti ya msalaba!
9Kwa hiyo, Mungu alimtukuza juu sana,
na kumpa Jina lililo kuu kuliko kila jina,
10ili kwa Jina la Isa, kila goti lipigwe,
la vitu vya mbinguni, na vya duniani,
na vya chini ya nchi,
11na kila ulimi ukiri kwamba
Isa Al-Masihi ni Bwana,
kwa utukufu wa Mungu Baba Mwenyezi.
Ng’aeni kama mianga katika ulimwengu
12Kwa hiyo, wapendwa wangu, kama vile mmekuwa mkitii siku zote, si tu wakati nikiwa pamoja nanyi, bali sasa zaidi sana nisipokuwepo, utimizeni wokovu wenu kwa kuogopa na kutetemeka, 13kwa maana Mungu ndiye atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu kwa kulitimiza kusudi lake jema.
14Fanyeni mambo yote bila kunung’unika wala kushindana, 15ili msiwe na lawama wala hatia, bali mwe wana wa Mungu wasio na kasoro katika kizazi chenye ukaidi na kilichopotoka, ambacho ndani yake ninyi mnang’aa kama mianga ulimwenguni. 16Mkilishika neno la uzima, ili nipate kuona fahari siku ya Al-Masihi kwamba sikupiga mbio wala kujitaabisha bure. 17Lakini hata nikimiminwa kama sadaka ya kinywaji kwenye dhabihu na huduma inayotoka katika imani yenu, mimi ninafurahi na kushangilia pamoja nanyi nyote. 18Vivyo hivyo, ninyi nanyi imewapasa kufurahi na kushangilia pamoja nami.
Paulo amsifu Timotheo
19Natumaini katika Bwana Isa kumtuma Timotheo hivi karibuni aje kwenu, ili nipate kufarijika moyo nitakapopata habari zenu. 20Sina mtu mwingine kama yeye, ambaye ataangalia hali yenu kwa halisi. 21Kwa maana kila mmoja anajishughulisha zaidi na mambo yake mwenyewe wala si yale ya Isa Al-Masihi. 22Lakini ninyi wenyewe mnajua jinsi Timotheo alivyojithibitisha mwenyewe, kwa maana ametumika pamoja nami kwa kazi ya Injili, kama vile mwana kwa baba yake. 23Kwa hiyo, ninatumaini kumtuma kwenu upesi mara nitakapojua mambo yangu yatakavyokuwa. 24Nami mwenyewe ninatumaini katika Bwana Isa kwamba nitakuja kwenu hivi karibuni.
Paulo amsifu Epafrodito
25Lakini nadhani ni muhimu kumtuma tena kwenu Epafrodito, ndugu yangu na mtendakazi pamoja nami, aliye askari mwenzangu, ambaye pia ni mjumbe wenu mliyemtuma ili ashughulike na mahitaji yangu. 26Kwa maana amekuwa akiwaonea sana shauku ninyi nyote, akiwa na wasiwasi kwa kuwa mlisikia kwamba alikuwa mgonjwa. 27Kweli alikuwa mgonjwa, tena karibu ya kufa. Lakini Mungu alimhurumia, wala si yeye tu, bali hata na mimi alinihurumia, nisipatwe na huzuni juu ya huzuni. 28Kwa hiyo mimi ninafanya bidii kumtuma kwenu ili mtakapomwona kwa mara nyingine, mpate kufurahi, nami wasiwasi wangu upungue. 29Kwa hiyo mpokeeni katika Bwana Isa kwa furaha kubwa, nanyi wapeni heshima watu kama hawa, 30kwa sababu alikaribia kufa kwa ajili ya kazi ya Al-Masihi, akihatarisha maisha yake ili aweze kunihudumia vile ninyi hamkuweza.