Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mithali 23

23
Msemo 7
1Uketipo kula chakula na mtawala,
angalia vyema kile kilicho mbele yako,
2na utie kisu kooni mwako
kama ukiwa mlafi.
3Usitamani vyakula vyake vitamu
kwa kuwa chakula hicho ni cha hila.
Msemo 8
4Usijitaabishe ili kuupata utajiri,
uwe na hekima kuonesha kujizuia.
5Kufumba na kufumbua utajiri hutoweka,
huwa kama umepata mabawa ghafula,
ukaruka na kutoweka angani kama tai.
Msemo 9
6Usile chakula cha mtu mchoyo,
usitamani vyakula vyake vitamu,
7kwa maana yeye ni aina ya mtu
ambaye kila mara anafikiri kuhusu gharama.
Anakuambia, “Kula na kunywa,”
lakini moyo wake hauko pamoja nawe.
8Utatapika kile kidogo ulichokula,
nawe utakuwa umepoteza bure
maneno yako ya kumsifu.
Msemo 10
9Usizungumze na mpumbavu,
kwa maana atadhihaki hekima ya maneno yako.
Msemo 11
10Usisogeze jiwe la mpaka wa zamani
wala kunyemelea kwenye mashamba ya yatima,
11kwa kuwa Mtetezi wao ni mwenye nguvu,
atawatetea dhidi yako.
Msemo 12
12Elekeza moyo wako kwenye mafundisho
na masikio yako kwenye maneno ya maarifa.
Msemo 13
13Usimnyime mtoto adhabu,
ukimwadhibu kwa fimbo, hatakufa.
14Mwadhibu kwa fimbo
na kuiokoa nafsi yake kutoka mautini#23:14 mautini maana yake ni Kuzimu.
Msemo 14
15Mwanangu, kama moyo wako una hekima,
basi moyo wangu utafurahi,
16utu wangu wa ndani utafurahi,
wakati midomo yako
itakapozungumza lililo sawa.
Msemo 15
17Usiuruhusu moyo wako kuwaonea wivu wenye dhambi,
bali kila mara uwe na bidii katika kumcha Mwenyezi Mungu.
18Hakika kuna tumaini la baadaye kwa ajili yako,
nalo tarajio lako halitakatiliwa mbali.
Msemo 16
19Sikiliza, mwanangu na uwe na hekima,
weka moyo wako kwenye njia iliyo sawa.
20Usiwe miongoni mwa wanywao mvinyo,
au wale walao nyama kwa pupa,
21kwa maana walevi na walafi huwa maskini,
nako kusinzia huwavika matambara.
Msemo 17
22Msikilize baba yako, aliyekuzaa,
wala usimdharau mama yako atakapokuwa mzee.
23Nunua kweli wala usiiuze,
pata hekima, adabu na ufahamu.
24Baba wa mwenye haki ana furaha kubwa,
naye aliye na mwana mwenye hekima humfurahia.
25Baba yako na mama yako na wafurahi,
mama aliyekuzaa na ashangilie!
Msemo 18
26Mwanangu, nipe moyo wako,
macho yako na yafuate njia zangu,
27kwa maana kahaba ni shimo refu
na mwanamke mpotovu ni kisima chembamba.
28Kama mnyang’anyi, hungojea akivizia,
naye huzidisha wasio waaminifu miongoni mwa wanaume.
Msemo 19
29Ni nani mwenye ole?
Ni nani mwenye huzuni?
Ni nani mwenye ugomvi?
Ni nani mwenye malalamiko?
Ni nani aliye na majeraha yasiyo na sababu?
Ni nani mwenye macho mekundu?
30Ni hao wanaokaa sana kwenye mvinyo,
hao wanaoenda kuonja mabakuli ya mvinyo uliochanganywa.
31Usiukodolee macho mvinyo ukiwa mwekundu,
unapometameta kwenye bilauri,
unaposhuka taratibu!
32Mwishowe huuma kama nyoka
na kutia sumu yake kama nyoka mwenye sumu.
33Macho yako yataona mambo mageni,
na moyo wako kuwazia mambo yaliyopotoka.
34Utakuwa kama alalaye baharini,
alalaye juu ya kamba ya merikebu.
35Utasema, “Wamenipiga lakini sikuumia!
Wamenichapa, lakini sisikii!
Nitaamka lini
ili nikanywe tena?”

Iliyochaguliwa sasa

Mithali 23: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia