26
1Kama theluji wakati wa kiangazi au mvua wakati wa mavuno,
ndivyo asivyostahili heshima mpumbavu.
2Kama shomoro apigapigavyo mabawa yake
au mbayuwayu katika kuruka kwake kasi,
ndivyo ilivyo laana isiyo na sababu haimpati mtu.
3Mjeledi kwa farasi, lijamu kwa punda,
nayo fimbo kwa migongo ya wapumbavu!
4Usimjibu mpumbavu sawasawa na upumbavu wake,
ama wewe mwenyewe utakuwa kama yeye.
5Mjibu mpumbavu sawasawa na upumbavu wake,
ama atakuwa mwenye hekima machoni pake mwenyewe.
6Kama vile ilivyo kujikata miguu au kunywa sumu,
ndivyo ilivyo kutuma ujumbe kwa mkono wa mpumbavu.
7Kama miguu ya kiwete inavyoning’inia
ndivyo ilivyo mithali katika kinywa cha mpumbavu.
8Kama kufunga jiwe kwenye kombeo,
ndivyo ilivyo kumpa mpumbavu heshima.
9Kama mwiba kwenye mkono wa mlevi
ndivyo ilivyo mithali kinywani mwa mpumbavu.
10Kama mpiga upinde ambaye hujeruhi ovyo,
ndivyo alivyo yeye aajiriye mpumbavu au yeyote apitaye njiani.
11Kama mbwa ayarudiavyo matapiko yake,
ndivyo mpumbavu arudiavyo upumbavu wake.
12Je, unamwona mtu ajionaye mwenye hekima
machoni pake mwenyewe?
Liko tumaini zaidi kwa mpumbavu kuliko kwake.
13Mvivu husema, “Yuko simba barabarani,
simba mkali anazunguka mitaa!”
14Kama vile mlango ugeukavyo kwenye bawaba zake,
ndivyo mvivu ajigeuzavyo kitandani mwake.
15Mtu mvivu hutumbukiza mkono wake kwenye sahani,
naye huchoka kuupeleka kwenye kinywa chake.
16Mtu mvivu ni mwenye hekima machoni pake mwenyewe,
kuliko watu saba wawezao kujibu kwa busara.
17Kama yeye amkamataye mbwa kwa masikio,
ndivyo alivyo mtu apitaye njiani na kujiingiza kwenye ugomvi usiomhusu.
18Kama mwendawazimu
atupaye mishale ya moto ya kufisha,
19ndivyo alivyo mtu amdanganyaye jirani yake na kusema,
“Nilikuwa nikifanya mzaha tu!”
20Bila kuni moto huzimika;
pasipo uchongezi ugomvi humalizika.
21Kama makaa juu ya makaa yanayowaka,
na kama kuni kwenye moto,
ndivyo alivyo mtu mgomvi kwa kuchochea ugomvi.
22Maneno ya mchongezi ni kama chakula kitamu;
huingia sehemu za ndani sana za mtu.
23Kama rangi ing’aayo iliyopakwa kwenye vyombo vya udongo
ndivyo ilivyo midomo laini pamoja na moyo mbaya.
24Mtu mwenye nia ya kudhuru wengine hujificha kwa maneno ya midomo yake,
lakini moyoni mwake huficha udanganyifu.
25Ingawa maneno yake huvutia, usimwamini,
kwa maana machukizo saba hujaza moyo wake.
26Nia yake ya kudhuru wengine inaweza kufichwa na udanganyifu,
lakini uovu wake utafichuliwa kwenye kusanyiko.
27Mtu akichimba shimo, atatumbukia ndani yake;
mtu akivingirisha jiwe, litamrudia.
28Ulimi wa uongo huwachukia wale unaowaumiza,
nacho kinywa cha kujipendekeza husababisha uharibifu.