Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mithali 3

3
Faida nyingine za hekima
1Mwanangu, usisahau mafundisho yangu,
bali zitunze amri zangu moyoni mwako,
2kwa kuwa zitakuongezea miaka mingi ya maisha yako
na kukuletea mafanikio.
3Usiache kamwe upendo na uaminifu vitengane nawe;
vifunge shingoni mwako,
viandike katika ubao wa moyo wako.
4Ndipo utapata kibali na jina zuri
mbele za Mungu na mwanadamu.
5Mtumaini Mwenyezi Mungu kwa moyo wako wote
wala usizitegemee akili zako mwenyewe;
6katika njia zako zote mkiri yeye,
naye atayanyoosha mapito yako.
7Usiwe mwenye hekima machoni pako mwenyewe;
mche Mwenyezi Mungu ukajiepushe na uovu.
8Hii itakuletea afya mwilini mwako,
na lishe kwenye mifupa yako.
9Mheshimu Mwenyezi Mungu kwa mali yako
na kwa malimbuko ya mazao yako yote;
10ndipo ghala zako zitakapojaa hadi kufurika,
viriba vyako vitafurika kwa mvinyo mpya.
11Mwanangu, usidharau adhabu ya Mwenyezi Mungu
na usichukie maonyo yake,
12kwa sababu Mwenyezi Mungu huwaadibisha wale anaowapenda,
kama vile baba afanyavyo
kwa mwana apendezwaye naye.
13Heri mtu yule apataye hekima,
mtu yule apataye ufahamu,
14kwa maana hekima ana faida kuliko fedha
na mapato yake ni bora kuliko ya dhahabu safi.
15Hekima ana thamani kuliko marijani;
hakuna chochote unachokitamani
kinachoweza kulinganishwa naye.
16Maisha marefu yako katika mkono wake wa kuume;
katika mkono wake wa kushoto
kuna utajiri na heshima.
17Njia zake zinapendeza,
mapito yake yote ni amani.
18Yeye ni mti wa uzima kwa wale wanaomkumbatia;
wale wamshikao watabarikiwa.
19Kwa hekima Mwenyezi Mungu aliiweka misingi ya dunia,
kwa ufahamu aliziweka mbingu mahali pake;
20kwa maarifa yake vilindi viligawanywa,
nayo mawingu yanadondosha umande.
21Mwanangu, hifadhi maamuzi mema na busara,
usiache vitoke machoni pako;
22ndipo vitakapokuwa uzima nafsini mwako
na pambo la neema shingoni mwako.
23Kisha utaenda katika njia yako salama,
wala mguu wako hautajikwaa;
24unapolala, hutaogopa;
unapolala, usingizi wako utakuwa mtamu.
25Usiogope maafa ya ghafula
au maangamizi yanayowapata waovu,
26kwa kuwa Mwenyezi Mungu atakuwa tumaini lako
na kuepusha mguu wako kunaswa katika mtego.
27Usizuie wema kwa wale wanaostahili
ikiwa katika uwezo wako kutenda.
28Usimwambie jirani yako,
“Njoo baadaye, nitakupa kesho”:
wakati wewe unacho kitu kile karibu nawe.
29Usipange mabaya dhidi ya jirani yako,
anayeishi karibu nawe kwa uaminifu.
30Usimshtaki mtu bila sababu,
wakati hajakudhuru kwa lolote.
31Usimwonee wivu mtu mwenye jeuri
wala kuchagua njia yake yoyote,
32kwa kuwa Mwenyezi Mungu humchukia mtu mpotovu,
lakini siri yake iko kwa mwenye haki.
33Laana ya Mwenyezi Mungu i juu ya nyumba ya mwovu,
lakini yeye huibariki nyumba ya mwenye haki.
34Huwadhihaki wale wanaodhihaki,
lakini huwapa neema wale wanyenyekevu na walioonewa.
35Wenye hekima hurithi heshima,
bali huwaaibisha wapumbavu.

Iliyochaguliwa sasa

Mithali 3: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia