Mithali Utangulizi
Utangulizi
Neno la Kiebrania “Mashal” ndilo lililotafsiriwa “Mithali”; lina maana nyingine zaidi, yaani “Mapokeo”, “Mafumbo”, au “Semi za hekima”. Hivyo, kitabu cha Mithali ni mkusanyiko wa semi nyingi za hekima, busara, na mambo yanayohusu haki katika maisha ya kila siku katika jamii.
Kitabu hiki kimejaa mafundisho yenye mafumbo yaliyokuwa ya kawaida katika mazingira ya Mashariki ya Kati nyakati zile. Mambo ya hekima yaliyo katika kitabu hiki ni ya kipekee sana kwa sababu yameelezwa kwa mtazamo wa Mwenyezi Mungu kwa kutumia vigezo vya haki. Kitabu cha Mithali kimekuwa tunu na msaada mkubwa katika kutoa mafundisho ya kuwaongoza watu kutenda mambo kwa hekima na busara.
Kama vile Daudi alivyo chimbuko la Zaburi katika Israeli, ndivyo Sulemani alivyo chimbuko la hekima katika Israeli (1:1; 10:1; 25:1).
Mwandishi
Inadhaniwa kuwa mwandishi ni zaidi ya mtu mmoja: Sulemani, Aguri mwana wa yake, Mfalme Lemueli, na wenye hekima ambao majina yao hayakutajwa. Maandishi yalikusanywa na kuwekwa pamoja wakati wa Mfalme Hezekia.
Kusudi
Kuwafundisha watu jinsi ya kupata hekima, kuishi maisha ya uadilifu, kutenda haki, na jinsi ya kutambua tofauti kati ya wema na uovu, kweli na uongo, hekima na upumbavu; kuwaelekeza na kuwahimiza watu kuishi maisha ya kumtii Mwenyezi Mungu ambaye ndiye chanzo na utoshelevu wa maarifa na ufahamu kamilifu.
Mahali
Yerusalemu.
Tarehe
Maandiko ya kitabu hiki yalikusanywa pamoja na Mfalme Hezekia mnamo 715–686 K.K.
Wahusika Wakuu
Sulemani, Aguri na Lemueli.
Wazo Kuu
Kumcha Mwenyezi Mungu ni chanzo cha maarifa.
Mambo Muhimu
Baadhi ya mambo muhimu yaliyoorodheshwa katika kitabu hiki ni: Vijana na nidhamu, jamaa, kumjua Mwenyezi Mungu, ndoa, kufahamu ukweli na hekima.
Yaliyomo
Utangulizi, na maelezo juu ya hekima na upumbavu (1:1–9:18)
Mithali za Sulemani (10:1–22:16)
Misemo ya wenye hekima (22:17–24:34)
Mithali zaidi za Sulemani (25:1–29:27)
Misemo ya Aguri na ya Lemueli (30:1–31:9)
Mke mwenye sifa nzuri (31:10-31).
Iliyochaguliwa sasa
Mithali Utangulizi: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapistaging.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.