Zaburi 118
118
Zaburi 118
Shukrani kwa ajili ya ushindi
1Mshukuruni Mwenyezi Mungu, kwa kuwa ni mwema;
fadhili zake zadumu milele.
2Israeli na aseme sasa:
“Fadhili zake zadumu milele.”
3Nyumba ya Haruni na iseme sasa:
“Fadhili zake zadumu milele.”
4Wote wanaomcha Mwenyezi Mungu na waseme sasa:
“Fadhili zake zadumu milele.”
5Wakati wa maumivu yangu makuu, nilimlilia Mwenyezi Mungu,
naye akanijibu kwa kuniweka huru.
6Mwenyezi Mungu yuko pamoja nami, sitaogopa.
Mwanadamu anaweza kunitenda nini?
7Mwenyezi Mungu yuko pamoja nami,
yeye ni msaidizi wangu.
Nitawatazama adui zangu
wakiwa wameshindwa.
8Ni bora kumkimbilia Mwenyezi Mungu
kuliko kumtumainia mwanadamu.
9Ni bora kumkimbilia Mwenyezi Mungu
kuliko kuwatumainia wakuu.
10Mataifa yote yalinizunguka,
lakini kwa jina la Mwenyezi Mungu naliwakatilia mbali.
11Walinizunguka pande zote,
lakini kwa jina la Mwenyezi Mungu naliwakatilia mbali.
12Walinizunguka kama kundi la nyuki,
lakini walikufa haraka kama miiba iteketeayo;
kwa jina la Mwenyezi Mungu naliwakatilia mbali.
13Nilisukumwa nyuma karibu kuanguka,
lakini Mwenyezi Mungu alinisaidia.
14Mwenyezi Mungu ni nguvu yangu na wimbo wangu,
yeye amefanyika wokovu wangu.
15Sauti za shangwe na ushindi
zinavuma kwenye hema za wenye haki:
“Mkono wa kuume wa Mwenyezi Mungu
umetenda mambo makuu!
16Mkono wa kuume wa Mwenyezi Mungu
umeinuliwa juu,
mkono wa kuume wa Mwenyezi Mungu
umetenda mambo makuu!”
17Sitakufa, bali nitaishi,
nami nitayatangaza matendo ya Mwenyezi Mungu.
18Mwenyezi Mungu ameniadhibu vikali,
lakini hakuniacha nife.
19Nifungulie malango ya haki,
nami nitaingia na kumshukuru Mwenyezi Mungu.
20Hili ni lango la Mwenyezi Mungu
ambalo wenye haki wanaweza kuliingia.
21Nitakushukuru, kwa kuwa ulinijibu,
umekuwa wokovu wangu.
22Jiwe walilolikataa waashi,
limekuwa jiwe kuu la pembeni.
23Mwenyezi Mungu ametenda hili,
nalo ni la kushangaza machoni petu.
24Hii ndiyo siku Mwenyezi Mungu aliyoifanya,
tushangilie na kufurahi ndani yake.
25Ee Mwenyezi Mungu, tuokoe,
Ee Mwenyezi Mungu, utujalie mafanikio.
26Heri yule ajaye kwa jina la Mwenyezi Mungu.
Kutoka nyumba ya Mwenyezi Mungu tunakubariki.
27Mwenyezi Mungu ndiye Mungu,
naye ametuangazia nuru yake.
Mkiwa na matawi mkononi,
unganeni kwenye maandamano ya sikukuu
hadi kwenye pembe za madhabahu.
28Wewe ni Mungu wangu, nitakushukuru,
wewe ni Mungu wangu, nitakutukuza.
29Mshukuruni Mwenyezi Mungu kwa kuwa ni mwema;
fadhili zake zadumu milele.
Iliyochaguliwa sasa
Zaburi 118: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapistaging.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.