Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 139:13-24

Zaburi 139:13-24 NEN

Kwa maana wewe ndiwe uliyeumba utu wangu wa ndani; uliniunga pamoja tumboni mwa mama yangu. Ninakusifu kwa sababu nimeumbwa kwa namna ya ajabu na ya kutisha; kazi zako ni za ajabu, ninajua hayo kikamilifu. Umbile langu halikufichika kwako, nilipoumbwa mahali pa siri. Nilipoungwa pamoja kwa ustadi katika vilindi vya nchi, macho yako yaliniona kabla mwili wangu haujakamilika. Siku zangu zote ulizonipangia ziliandikwa katika kitabu chako kabla haijakuwepo hata moja. Tazama jinsi yalivyo ya thamani mawazo yako kwangu, Ee Mungu! Jinsi jumla yake ilivyo kubwa! Kama ningezihesabu, zingekuwa nyingi kuliko mchanga. Niamkapo, bado niko pamoja nawe. Laiti ungewachinja waovu, Ee Mungu! Ondokeni kwangu, ninyi wamwaga damu! Wanazungumza juu yako wakiwa na kusudi baya, adui zako wanatumia vibaya jina lako. Ee BWANA, je, nisiwachukie wanaokuchukia? Nisiwachukie sana wanaoinuka dhidi yako? Sina kitu zaidi ya chuki dhidi yao, ninawahesabu ni adui zangu. Ee Mungu, nichunguze, uujue moyo wangu, nijaribu na ujue mawazo yangu. Uone kama kuna njia iletayo machukizo ndani yangu, uniongoze katika njia ya milele.