Zaburi 18
18
Zaburi 18
Wimbo Wa Daudi Wa Ushindi
(2 Samweli 22:1-51)
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi mtumishi wa Bwana aliyomwimbia Bwana wakati Bwana alipomwokoa mikononi mwa adui zake wote, na pia mkononi mwa Sauli. Alisema hivi:
1 Nakupenda wewe, Ee Bwana,
nguvu yangu.
2 Bwana ni mwamba wangu,
ngome yangu na mwokozi wangu,
Mungu wangu ni mwamba,
ambaye kwake ninakimbilia.
Yeye ni ngao yangu na pembe ya wokovu wangu,
ngome yangu.
3 Ninamwita Bwana anayestahili kusifiwa,
nami ninaokolewa kutoka kwa adui zangu.
4 Kamba za mauti zilinizunguka,
mafuriko ya maangamizi yalinilemea.
5 Kamba za kuzimu zilinizunguka,
mitego ya mauti ilinikabili.
6 Katika shida yangu nalimwita Bwana,
nilimlilia Mungu wangu anisaidie.
Kutoka hekaluni mwake alisikia sauti yangu,
kilio changu kikafika mbele zake,
masikioni mwake.
7 Dunia ilitetemeka na kutikisika,
misingi ya milima ikatikisika,
vilitetemeka kwa sababu alikuwa amekasirika.
8 Moshi ukapanda kutoka puani mwake,
moto uteketezao ukatoka kinywani mwake,
makaa ya moto yawakayo
yakatoka ndani mwake.
9 Akazipasua mbingu akashuka chini,
mawingu meusi yalikuwa chini ya miguu yake.
10 Alipanda juu ya kerubi akaruka,
akapaa juu kwa mbawa za upepo.
11 Alifanya giza kuwa kitu chake cha kujifunika,
hema lake kumzunguka,
mawingu meusi ya mvua ya angani.
12 Kutokana na mwanga wa uwepo wake
mawingu yalisogea,
ikanyesha mvua ya mawe
na umeme wa radi.
13 Bwana alinguruma kutoka mbinguni,
sauti ya Aliye Juu Sana ilisikika.
14 Aliipiga mishale yake na kutawanya adui,
naam, umeme mwingi wa radi na kuwafukuza.
15 Mabonde ya bahari yalifunuliwa,
na misingi ya dunia ikawa wazi
kwa kukaripia kwako, Ee Bwana,
kwa uvumi wa pumzi kutoka puani mwako.
16 Alinyoosha mkono kutoka juu na kunishika;
alinitoa kutoka kilindi cha maji makuu.
17 Aliniokoa kutoka adui wangu mwenye nguvu nyingi,
kutoka adui zangu waliokuwa na nguvu nyingi kuliko mimi.
18 Walinikabili siku ya msiba wangu,
lakini Bwana alikuwa msaada wangu.
19 Alinileta nje mahali penye nafasi tele,
akaniokoa kwa kuwa alipendezwa nami.
20 Bwana alinitendea sawasawa na uadilifu wangu;
sawasawa na usafi wa mikono yangu amenilipa.
21 Kwa maana nimezishika njia za Bwana;
sijatenda ubaya nikamwacha Mungu wangu.
22 Sheria zake zote zi mbele yangu,
wala sijayaacha maagizo yake.
23 Nimekuwa sina hatia mbele zake,
nami nimejilinda nisitende dhambi.
24 Bwana amenilipa sawasawa na uadilifu wangu;
sawasawa na usafi wa mikono yangu machoni pake.
25 Kwa yeye aliye mwaminifu, unajionyesha kuwa mwaminifu,
kwa asiye na hatia, unajionyesha kutokuwa na hatia.
26 Kwa aliye mtakatifu, unajionyesha kuwa mtakatifu,
lakini kwa aliyepotoka, unajionyesha kuwa mkaidi.
27 Wewe huwaokoa wanyenyekevu,
lakini huwashusha wenye kiburi.
28 Wewe, Ee Bwana, unaifanya taa yangu iendelee kuwaka;
Mungu wangu hulifanya giza langu kuwa mwanga.
29 Kwa msaada wako naweza kushinda jeshi,
nikiwa pamoja na Mungu wangu
nitaweza kuruka ukuta.
30 Kuhusu Mungu, njia yake ni kamilifu,
neno la Bwana halina dosari.
Yeye ni ngao kwa wote
wanaokimbilia kwake.
31 Kwa maana ni nani aliye Mungu
zaidi ya Bwana?
Ni nani aliye Mwamba
isipokuwa Mungu wetu?
32 Mungu ndiye anivikaye nguvu
na kufanya njia yangu kuwa kamilifu.
33 Huifanya miguu yangu kama miguu ya kulungu,
huniwezesha kusimama mahali palipo juu.
34 Huifundisha mikono yangu kupigana vita;
mikono yangu inaweza kupinda upinde wa shaba.
35 Hunipa ngao yako ya ushindi,
nao mkono wako wa kuume hunitegemeza,
unajishusha chini ili kuniinua.
36 Huyapanua mapito yangu,
ili miguu yangu isiteleze.
37 Niliwafuatia adui zangu na nikawapata,
sikurudi nyuma mpaka walipoangamizwa.
38 Niliwaseta hata hawakuweza kuinuka tena;
walianguka chini ya miguu yangu.
39 Ulinivika nguvu kwa ajili ya kupigana vita;
uliwafanya adui zangu wasujudu miguuni pangu.
40 Uliwafanya adui zangu wageuke na kukimbia,
nami nikawaangamiza adui zangu.
41 Walipiga yowe, lakini hapakuwepo na yeyote wa kuwaokoa;
walimlilia Bwana, lakini hakuwajibu.
42 Niliwaponda kama mavumbi yanayopeperushwa na upepo;
niliwamwaga nje kama tope barabarani.
43 Umeniokoa kutokana na mashambulizi ya watu;
umenifanya kuwa kiongozi wa mataifa,
watu ambao sikuwajua wananitumikia.
44 Mara wanisikiapo hunitii,
wageni hunyenyekea mbele yangu.
45 Wote wanalegea,
wanatoka katika ngome zao wakitetemeka.
46 Bwana yu hai! Sifa ni kwa Mwamba wangu!
Atukuzwe Mungu Mwokozi wangu!
47 Yeye ndiye Mungu anilipiziaye kisasi,
awatiishaye mataifa chini yangu,
48 aniokoaye na adui zangu.
Uliniinua juu ya adui zangu;
uliniokoa toka kwa watu wajeuri.
49 Kwa hiyo nitakusifu katikati ya mataifa, Ee Bwana;
nitaliimbia sifa jina lako.
50 Humpa mfalme wake ushindi mkuu,
huonyesha fadhili zake kwa mpakwa mafuta wake,
kwa Daudi na wazao wake milele.
Iliyochaguliwa sasa
Zaburi 18: NEN
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Biblia Takatifu™ Neno™
Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Version™
Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 by Biblica, Inc.
Used with Permission. All Rights Reserved Worldwide.