25
Zaburi 25#25 Zaburi hii imetungwa kila mstari ukianzia na herufi ya alfabeti ya Kiebrania zikifuatana tangu Aleph (A) hadi Taw (T); zote ni 22.
Kumwomba Mwenyezi Mungu uongozi na ulinzi
Zaburi ya Daudi.
1Kwako wewe, Ee Mwenyezi Mungu,
naweka tumaini yangu.
2Ni wewe ninayekutumainia,
Usiniache niaibike,
wala adui zangu wanishinde.
3Kamwe hakuna hata mmoja anayekutegemea
atakayeaibishwa,
bali wataaibishwa
wafanyao hila bila sababu.
4Nioneshe njia zako, Ee Mwenyezi Mungu,
nifundishe mapito yako,
5niongoze katika kweli yako na kunifundisha,
kwa maana wewe ni Mungu Mwokozi wangu,
nalo tumaini langu liko kwako wakati wote.
6Kumbuka, Ee Mwenyezi Mungu, rehema zako kuu na upendo,
kwa maana zimekuwepo tangu zamani.
7Usizikumbuke dhambi za ujana wangu
wala njia zangu za uasi,
sawasawa na upendo wako unikumbuke,
kwa maana wewe ni mwema, Ee Mwenyezi Mungu.
8Mwenyezi Mungu ni mwema na mwenye adili,
kwa hiyo huwafundisha wenye dhambi njia zake.
9Huwaongoza wanyenyekevu katika haki,
naye huwafundisha njia yake.
10Njia zote za Mwenyezi Mungu ni za upendo na uaminifu
kwa wale wanaoshika shuhuda za agano lake.
11Ee Mwenyezi Mungu, kwa ajili ya jina lako,
unisamehe uovu wangu, ijapokuwa ni mwingi.
12Ni nani basi, mtu yule anayemcha Mwenyezi Mungu?
Atamfundisha katika njia
atakayoichagua kwa ajili yake.
13Mtu huyo atafanikiwa maishani mwake,
nao wazao wake watairithi nchi.
14Siri ya Mwenyezi Mungu iko kwa wale wamchao,
yeye huwajulisha agano lake.
15Macho yangu humwelekea Mwenyezi Mungu daima,
kwa kuwa yeye peke yake ndiye ataitoa
miguu yangu kutoka mtego.
16Nigeukie na unihurumie,
kwa maana mimi ni mpweke na mwenye kuteseka.
17Shida za moyo wangu zimeongezeka,
niokoe katika dhiki yangu.
18Uangalie mateso na shida zangu
na uniondolee dhambi zangu zote.
19Tazama adui zangu walivyo wengi,
pia uone jinsi wanavyonichukia vikali!
20Uyalinde maisha yangu na uniokoe,
usiniache niaibike,
kwa maana nimekukimbilia wewe.
21Uadilifu na uaminifu vinilinde,
kwa sababu tumaini langu ni kwako, Mwenyezi Mungu.
22Ee Mungu, wakomboe Israeli,
katika shida zao zote!