Zaburi 28:1-9
Zaburi 28:1-9 NENO
Ninakuita wewe, Ee Mwenyezi Mungu, Mwamba wangu; usikatae kunisikiliza. Kwa sababu ukinyamaza nitafanana na walioshuka shimoni. Sikia kilio changu nikikuomba unihurumie, ninapokuita ili unisaidie, ninapoinua mikono yangu kuelekea Patakatifu pa Patakatifu pako. Usiniburute pamoja na waovu, pamoja na hao watendao mabaya, ambao huzungumza na majirani zao maneno mazuri, lakini mioyoni mwao wameficha chuki. Walipe sawasawa na matendo yao, sawasawa na matendo yao maovu; walipe sawasawa na kazi za mikono yao, uwalipe wanavyostahili. Kwa kuwa hawaheshimu kazi za Mwenyezi Mungu, na yale ambayo mikono yake imetenda, atawabomoa na kamwe hatawajenga tena. Ahimidiwe Mwenyezi Mungu, kwa maana amesikia kilio changu nikimwomba anihurumie. Mwenyezi Mungu ni nguvu zangu na ngao yangu, moyo wangu umemtumaini yeye, nami nimesaidiwa. Moyo wangu unarukaruka kwa furaha nami nitamshukuru kwa wimbo. Mwenyezi Mungu ni nguvu ya watu wake, ngome ya wokovu kwa mpakwa mafuta wake. Waokoe watu wako na uubariki urithi wako; uwe mchungaji wao na uwabebe milele.