Zaburi 28:1-9
Zaburi 28:1-9 SRUV
Ee BWANA, nitakuita Ewe, mwamba wangu, Usiwe kwangu kama kiziwi. Nisije nikafanana nao washukao shimoni, Ikiwa umeninyamalia. Uisikie sauti ya dua yangu nikuombapo, Nikipainulia patakatifu pako mikono yangu. Usinikokote pamoja na wasio haki, Wala pamoja na watenda maovu. Wawaambiao jirani zao maneno ya amani, Lakini mioyoni mwao mna madhara. Uwape sawasawa na vitendo vyao, Na kwa kadiri ya uovu wa matendo yao, Uwape sawasawa na kazi ya mikono yao, Uwalipe kile wanachostahili. Maana hawazifahamu kazi za BWANA, Wala matendo ya mikono yake, Atawavunja wala hatawajenga tena; Na ahimidiwe BWANA. Maana ameisikia sauti ya dua yangu; BWANA ni nguvu zangu na ngao yangu. Moyo wangu umemtumaini, Nami nimesaidiwa; Basi, moyo wangu unashangilia, Na kwa wimbo wangu nitamshukuru. BWANA ni nguvu za watu wake, Naye ni ngome ya wokovu kwa masihi wake. Uwaokoe watu wako, uubariki urithi wako, Uwachunge, uwachukue milele.