Zaburi 34:11-22
Zaburi 34:11-22 NEN
Njooni, watoto wangu, mnisikilize, nitawafundisha kumcha BWANA. Yeyote kati yenu anayependa uzima na kutamani kuziona siku nyingi njema, basi auzuie ulimi wake na mabaya, na midomo yake kutokana na kusema uongo. Aache uovu, atende mema, aitafute amani na kuifuatilia. Macho ya BWANA huwaelekea wenye haki, na masikio yake yako makini kusikiliza kilio chao. Uso wa BWANA uko kinyume na watendao maovu, ili kufuta kumbukumbu lao duniani. Wenye haki hulia, naye BWANA huwasikia, huwaokoa katika taabu zao zote. BWANA yu karibu na waliovunjika moyo, na huwaokoa waliopondeka roho. Mwenye haki ana mateso mengi, lakini BWANA humwokoa nayo yote, huhifadhi mifupa yake yote, hata mmoja hautavunjika. Ubaya utamuua mtu mwovu, nao adui za mwenye haki watahukumiwa. BWANA huwakomboa watumishi wake, yeyote anayemkimbilia yeye hatahukumiwa kamwe.