Zaburi 34:11-22
Zaburi 34:11-22 Biblia Habari Njema (BHN)
Njoni enyi vijana mkanisikilize, nami nitawafundisha kumcha Mwenyezi-Mungu. Je, watamani kufurahia maisha, kuishi maisha marefu na kufurahia mema? Basi, acha kusema mabaya, na kuepa kusema uongo. Jiepushe na uovu, utende mema; utafute amani na kuizingatia. Mwenyezi-Mungu huwaangalia waadilifu, na kusikiliza malalamiko yao; lakini huwapinga watu watendao maovu, awafutilie mbali kutoka duniani. Waadilifu wakimlilia Mwenyezi-Mungu yeye huwasikia, na kuwaokoa katika taabu zao zote. Mwenyezi-Mungu yu karibu na waliokufa moyo; huwaokoa wote waliokata tamaa kabisa. Mateso ya mwadilifu ni mengi, lakini Mwenyezi-Mungu humwokoa kutoka yote. Huvilinda viungo vya mwili wake wote, hakuna hata mfupa wake mmoja utakaovunjwa. Ubaya huwaletea waovu kifo; wanaowachukia waadilifu wataadhibiwa. Mwenyezi-Mungu huokoa maisha ya watumishi wake, wote wanaomkimbilia hawataadhibiwa.
Zaburi 34:11-22 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Njoni, enyi wana, mnisikilize, Nami nitawafundisha kumcha BWANA. Ni nani atamaniye uzima na atakaye kuishi, Siku nyingi afurahie mema? Uuzuie ulimi wako na mabaya, Na midomo yako na kusema hila. Uache mabaya ukatende mema, Utafute amani ukaifuatie. Macho ya BWANA huwaelekea wenye haki, Na masikio yake hukielekea kilio chao. Uso wa BWANA ni juu ya watenda mabaya, Aliondoe kumbukumbu lao duniani. Walilia, naye BWANA akasikia, Akawaponya kutoka kwa taabu zao zote. BWANA yu karibu nao waliovunjika moyo, Na huwaokoa waliopondeka roho. Mateso ya mwenye haki ni mengi, Lakini BWANA kutoka kwayo yote. Huihifadhi mifupa yake yote, Usivunjike hata mmoja. Uovu utamwua asiye haki, Nao wamchukiao mwenye haki watahukumiwa. BWANA huzikomboa nafsi za watumishi wake, Wote wamkimbiliao hawatahukumiwa.
Zaburi 34:11-22 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Njoni, enyi wana, mnisikilize, Nami nitawafundisha kumcha BWANA. Ni nani mtu yule apendezwaye na uzima, Apendaye siku nyingi apate kuona mema? Uuzuie ulimi wako na mabaya, Na midomo yako na kusema hila. Uache mabaya ukatende mema, Utafute amani ukaifuatie. Macho ya BWANA huwaelekea wenye haki, Na masikio yake hukielekea kilio chao. Uso wa BWANA ni juu ya watenda mabaya, Aliondoe kumbukumbu lao duniani. Walilia, naye BWANA akasikia, Akawaponya na taabu zao zote. BWANA yu karibu nao waliovunjika moyo, Na waliopondeka roho huwaokoa. Mateso ya mwenye haki ni mengi, Lakini BWANA humponya nayo yote. Huihifadhi mifupa yake yote, Haukuvunjika hata mmoja. Uovu utamwua asiye haki, Nao wamchukiao mwenye haki watahukumiwa. BWANA huzikomboa nafsi za watumishi wake, Wala hawatahukumiwa wote wamkimbiliao.
Zaburi 34:11-22 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Njooni, watoto wangu, mnisikilize, nitawafundisha kumcha BWANA. Yeyote kati yenu anayependa uzima na kutamani kuziona siku nyingi njema, basi auzuie ulimi wake na mabaya, na midomo yake kutokana na kusema uongo. Aache uovu, atende mema, aitafute amani na kuifuatilia. Macho ya BWANA huwaelekea wenye haki, na masikio yake yako makini kusikiliza kilio chao. Uso wa BWANA uko kinyume na watendao maovu, ili kufuta kumbukumbu lao duniani. Wenye haki hulia, naye BWANA huwasikia, huwaokoa katika taabu zao zote. BWANA yu karibu na waliovunjika moyo, na huwaokoa waliopondeka roho. Mwenye haki ana mateso mengi, lakini BWANA humwokoa nayo yote, huhifadhi mifupa yake yote, hata mmoja hautavunjika. Ubaya utamuua mtu mwovu, nao adui za mwenye haki watahukumiwa. BWANA huwakomboa watumishi wake, yeyote anayemkimbilia yeye hatahukumiwa kamwe.