Zaburi 62:1-12
Zaburi 62:1-12 NEN
Kwa Mungu peke yake nafsi yangu inapata pumziko; wokovu wangu watoka kwake. Yeye peke yake ndiye mwamba wangu na wokovu wangu; yeye ni ngome yangu, sitatikisika kamwe. Mtamshambulia mtu hata lini? Je, ninyi nyote mtamtupa chini, ukuta huu ulioinama na uzio huu unaotikisika? Walikusudia kikamilifu kumwangusha toka mahali pake pa fahari; wanafurahia uongo. Kwa vinywa vyao hubariki, lakini ndani ya mioyo yao hulaani. Ee nafsi yangu, upumzike, kwa Mungu peke yake, tumaini langu latoka kwake. Yeye peke yake ndiye mwamba wangu na wokovu wangu; ndiye ngome yangu, sitatikisika. Wokovu wangu na heshima yangu viko kwa Mungu, ndiye mwamba wangu wenye nguvu na kimbilio langu. Enyi watu, mtumainini yeye wakati wote, miminieni mioyo yenu kwake, kwa kuwa Mungu ni kimbilio letu. Binadamu wa ngazi ya chini ni pumzi tu, nao wa ngazi ya juu ni uongo tu; wakipimwa kwenye mizani, si chochote; wote kwa pamoja ni pumzi tu. Usitumainie vya udhalimu wala usijivune kwa vitu vya wizi; ingawa utajiri wako utaongezeka, usiviwekee moyo wako. Jambo moja Mungu amelisema, mambo mawili nimeyasikia: kwamba, Ee Mungu, wewe una nguvu, na kwamba, Ee BWANA, wewe ni mwenye upendo. Hakika utampa kila mtu thawabu kwa kadiri ya alivyotenda.