Zaburi 78:17-31
Zaburi 78:17-31 NEN
Lakini waliendelea kutenda dhambi dhidi yake, wakiasi jangwani dhidi ya Aliye Juu Sana. Kwa makusudi walimjaribu Mungu, wakidai vyakula walivyovitamani. Walinena dhidi ya Mungu, wakisema, “Je, Mungu aweza kuandaa meza jangwani? Alipopiga mwamba, maji yalitoka kwa nguvu, vijito vikatiririka maji mengi. Lakini je, aweza kutupa chakula pia? Je, anaweza kuwapa watu wake nyama?” BWANA alipowasikia, alikasirika sana, moto wake ukawa dhidi ya Yakobo, na ghadhabu yake ikawaka dhidi ya Israeli, kwa kuwa hawakumwamini Mungu, wala kuutumainia ukombozi wake. Hata hivyo alitoa amri kwa anga zilizo juu na kufungua milango ya mbingu, akawanyeshea mana ili watu wale; aliwapa nafaka ya mbinguni. Watu walikula mkate wa malaika, akawatumia chakula chote ambacho wangeliweza kula. Aliachia upepo wa mashariki kutoka kwenye mbingu na kuuongoza upepo wa kusini kwa uwezo wake. Aliwanyeshea nyama kama mavumbi, ndege warukao kama mchanga wa pwani. Aliwafanya washuke ndani ya kambi yao, kuzunguka mahema yao yote. Walikula na kusaza, kwa maana alikuwa amewapa kile walichotamani. Kabla hawajamaliza kula walichokitamani, hata kilipokuwa kingali bado vinywani mwao, hasira ya Mungu ikawaka juu yao, akawaua wale waliokuwa na nguvu zaidi miongoni mwao, akiwaangusha vijana wa Israeli.