Zaburi 78:17-31
Zaburi 78:17-31 Biblia Habari Njema (BHN)
Hata hivyo waliendelea kumkosea Mungu; walimwasi Mungu Mkuu kule jangwani. Walimjaribu Mungu kwa makusudi; wakidai wapewe chakula walichotaka. Walimkufuru Mungu wakisema: “Je, Mungu aweza kutupa chakula jangwani? Ni kweli, aliupiga mwamba, maji yakabubujika kama mto; lakini, sasa aweza kweli kutupatia mkate, na kuwapatia watu wake nyama?” Mwenyezi-Mungu, aliposikia hayo, alijawa na ghadhabu, moto ukawawakia wazawa wa Yakobo; hasira yake ikawavamia watu wa Israeli, kwa sababu hawakuwa na imani naye, wala hawakuamini nguvu yake ya kuokoa. Hata hivyo aliyaamuru mawingu ya juu, akaifungua milango ya mbingu; akawanyeshea mana wale, akawapa nafaka kutoka mbinguni. Binadamu, wakala chakula cha malaika; naye aliwapelekea chakula cha kutosha. Alivumisha upepo wa mashariki, kwa nguvu yake akachochea pepo za kusini; akawanyeshea watu wake nyama kama vumbi, ndege wengi kama mchanga wa pwani; ndege hao walianguka kambini mwao, kila mahali kuzunguka makao yao. Watu walikula wakashiba; Mungu aliwapa walichotaka. Lakini hata kabla ya kutosheleza hamu yao, chakula kikiwa bado mdomoni mwao, hasira ya Mungu iliwaka juu yao; akawaua wenye nguvu miongoni mwao, na kuwaangusha vijana wa Israeli.
Zaburi 78:17-31 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Lakini wakazidi kumtenda dhambi, Walipomwasi Aliye Juu katika jangwa. Wakamjaribu Mungu mioyoni mwao Kwa kutaka chakula kwa tamaa zao. Naam, walimwambia Mungu, wakasema, Je! Mungu aweza kuandaa meza jangwani? Tazama, aliupiga mwamba; Maji yakabubujika, ikafurika mito. Pia aweza kutupa chakula? Atawaandalia watu wake nyama? Hivyo BWANA aliposikia akaghadhibika; Moto ukawashwa juu ya Yakobo, Hasira nayo ikapanda juu ya Israeli. Kwa kuwa hawakumwamini Mungu, Wala hawakuutumainia wokovu wake. Lakini aliyaamuru mawingu juu; Akaifungua milango ya mbinguni; Akawanyeshea mana ili wale; Akawapa nafaka ya mbinguni. Mwanadamu akala chakula walacho malaika; Akawapelekea chakula cha kuwashibisha. Aliuelekeza upepo wa mashariki kuvuma toka mbinguni; Na kwa uweza wake akauongoza upepo wa kusini. Akawanyeshea nyama kama mavumbi, Na ndege wenye mbawa, Kama mchanga wa bahari. Akawaangusha kati ya matuo yao, Pande zote za maskani zao. Wakala wakashiba sana; Maana aliwaletea walivyovitamani; Lakini kabla ya kuitosheleza shauku yao, Huku chakula kikiwa bado kinywani mwao, Hasira ya Mungu ikapanda juu yao, Akawaua waliokuwa wanono; Akawaangusha chini vijana wa Israeli.
Zaburi 78:17-31 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Lakini wakazidi kumtenda dhambi, Walipomwasi Aliye juu katika nchi ya kiu. Wakamjaribu Mungu mioyoni mwao Kwa kutaka chakula kwa tamaa zao. Naam, walimwamba Mungu, wakasema, Je! Mungu aweza kuandika meza jangwani? Tazama, aliupiga mwamba; Maji yakabubujika, ikafurika mito. Pia aweza kutupa chakula? Atawaandalia watu wake nyama? Hivyo BWANA aliposikia akaghadhibika; Moto ukawashwa juu ya Yakobo, Hasira nayo ikapanda juu ya Israeli. Kwa kuwa hawakumwamini Mungu, Wala hawakuutumainia wokovu wake. Lakini aliyaamuru mawingu juu; Akaifungua milango ya mbinguni; Akawanyeshea mana ili wale; Akawapa nafaka ya mbinguni. Mwanadamu akala chakula cha mashujaa; Aliwapelekea chakula cha kuwashibisha. Aliuelekeza upepo wa mashariki mbinguni; Akaiongoza kusi kwa uweza wake. Akawanyeshea nyama kama mavumbi, Na ndege wenye mbawa, Kama mchanga wa bahari. Akawaangusha kati ya matuo yao, Pande zote za maskani zao. Wakala wakashiba sana; Maana aliwaletea walivyovitamani; Hawakuachana na matakwa yao. Ila chakula chao kikali ki vinywani mwao Hasira ya Mungu ikapanda juu yao, Akawaua waliokuwa wanono; Akawaangusha chini vijana wa Israeli.
Zaburi 78:17-31 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Lakini waliendelea kutenda dhambi dhidi yake, wakiasi jangwani dhidi ya Aliye Juu Sana. Kwa makusudi walimjaribu Mungu, wakidai vyakula walivyovitamani. Walinena dhidi ya Mungu, wakisema, “Je, Mungu aweza kuandaa meza jangwani? Alipopiga mwamba, maji yalitoka kwa nguvu, vijito vikatiririka maji mengi. Lakini je, aweza kutupa chakula pia? Je, anaweza kuwapa watu wake nyama?” BWANA alipowasikia, alikasirika sana, moto wake ukawa dhidi ya Yakobo, na ghadhabu yake ikawaka dhidi ya Israeli, kwa kuwa hawakumwamini Mungu, wala kuutumainia ukombozi wake. Hata hivyo alitoa amri kwa anga zilizo juu na kufungua milango ya mbingu, akawanyeshea mana ili watu wale; aliwapa nafaka ya mbinguni. Watu walikula mkate wa malaika, akawatumia chakula chote ambacho wangeliweza kula. Aliachia upepo wa mashariki kutoka kwenye mbingu na kuuongoza upepo wa kusini kwa uwezo wake. Aliwanyeshea nyama kama mavumbi, ndege warukao kama mchanga wa pwani. Aliwafanya washuke ndani ya kambi yao, kuzunguka mahema yao yote. Walikula na kusaza, kwa maana alikuwa amewapa kile walichotamani. Kabla hawajamaliza kula walichokitamani, hata kilipokuwa kingali bado vinywani mwao, hasira ya Mungu ikawaka juu yao, akawaua wale waliokuwa na nguvu zaidi miongoni mwao, akiwaangusha vijana wa Israeli.