Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 78

78
Zaburi 78
Mwenyezi Mungu na watu wake
Utenzi wa Asafu.
1Enyi watu wangu, sikieni mafundisho yangu,
sikilizeni maneno ya kinywa changu.
2Nitafungua kinywa changu kwa mafumbo,
nitazungumza mambo yaliyofichika, mambo ya kale:
3yale ambayo tuliyasikia na kuyajua,
yale ambayo baba zetu walituambia.
4Hatutayaficha kwa watoto wao;
tutakiambia kizazi kijacho
matendo yastahiliyo sifa ya Mwenyezi Mungu,
uweza wake, na maajabu aliyoyafanya.
5Aliagiza amri kwa Yakobo
na akaweka sheria katika Israeli,
ambazo aliwaamuru baba zetu
wawafundishe watoto wao,
6ili kizazi kijacho kizijue,
pamoja na watoto ambao watazaliwa,
nao pia wapate kuwaeleza watoto wao.
7Ndipo wangeweka tumaini lao kwa Mungu,
nao hawangesahau matendo yake,
bali wangezishika amri zake.
8Hawangefanana na baba zao,
waliokuwa kizazi cha ukaidi na uasi,
ambao roho zao hazikuwa na uaminifu kwa Mungu,
ambao roho zao hazikumwamini.
9Watu wa Efraimu, ingawa walijifunga pinde,
walikimbia siku ya vita.
10Hawakulishika agano la Mungu,
na walikataa kuishi kwa sheria yake.
11Walisahau aliyokuwa ameyatenda,
maajabu aliyokuwa amewaonesha.
12Alitenda miujiza machoni mwa baba zao,
huko Soani, katika nchi ya Misri.
13Aliigawanya bahari akawapitisha,
alifanya maji yasimame imara kama ukuta.
14Aliwaongoza kwa wingu mchana,
na kwa nuru ya moto usiku kucha.
15Alipasua miamba jangwani
na akawapa maji tele kama bahari,
16alitoa vijito kutoka jabali lililochongoka,
akayafanya maji yatiririke kama mito.
17Lakini waliendelea kutenda dhambi dhidi yake,
wakiasi jangwani dhidi ya Aliye Juu Sana.
18Kwa makusudi walimjaribu Mungu,
wakidai vyakula walivyovitamani.
19Walinena dhidi ya Mungu, wakisema,
“Je, Mungu aweza kuandaa meza jangwani?
20Alipopiga mwamba, maji yalitoka kwa nguvu,
vijito vikatiririka maji mengi.
Lakini je, aweza kutupatia chakula pia?
Je, anaweza kuwapatia watu wake nyama?”
21Mwenyezi Mungu alipowasikia, alikasirika sana,
moto wake ukawa dhidi ya Yakobo,
na ghadhabu yake ikawaka dhidi ya Israeli,
22kwa kuwa hawakumwamini Mungu,
wala kuutumainia ukombozi wake.
23Hata hivyo alitoa amri kwa anga zilizo juu
na kufungua milango ya mbingu,
24akawanyeshea mana ili watu wale;
aliwapa nafaka ya mbinguni.
25Watu walikula mkate wa malaika,
akawatumia chakula chote ambacho wangeweza kula.
26Aliachia upepo wa mashariki kutoka mbingu
na kuuongoza upepo wa kusini kwa uwezo wake.
27Aliwanyeshea nyama kama mavumbi,
ndege warukao kama mchanga wa pwani.
28Aliwafanya washuke ndani ya kambi yao,
kuzunguka mahema yao yote.
29Walikula na kusaza,
kwa maana alikuwa amewapa kile walichotamani.
30Kabla hawajamaliza kula walichokitamani,
hata kilipokuwa kingali bado vinywani mwao,
31hasira ya Mungu ikawaka juu yao,
akawaua wale waliokuwa na nguvu zaidi miongoni mwao,
akiwaangusha vijana wa Israeli.
32Licha ya haya yote, waliendelea kutenda dhambi,
licha ya maajabu yake, hawakuamini.
33Kwa hiyo akamaliza siku zao katika ubatili
na miaka yao katika vitisho.
34Kila mara Mungu alipowaua baadhi yao,
waliosalia walimtafuta,
walimgeukia tena kwa shauku.
35Walikumbuka kwamba Mungu alikuwa Mwamba wao,
kwamba Mungu Aliye Juu Sana alikuwa Mkombozi wao.
36Lakini walimdanganya kwa vinywa vyao,
wakisema uongo kwa ndimi zao,
37mioyo yao haikuwa thabiti kwake,
wala hawakuwa waaminifu katika agano lake.
38Hata hivyo alikuwa na huruma,
alisamehe maovu yao
na hakuwaangamiza.
Mara kwa mara alizuia hasira yake,
wala hakuchochea ghadhabu yake yote.
39Alikumbuka kwamba wao walikuwa nyama tu,
upepo upitao ambao haurudi.
40Mara ngapi walimwasi jangwani
na kumhuzunisha nyikani!
41Walimjaribu Mungu mara kwa mara,
wakamkasirisha yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli.
42Hawakukumbuka uwezo wake,
siku aliyowakomboa kutoka kwa mtesi,
43siku aliyoonesha ishara zake za ajabu huko Misri,
maajabu yake huko Soani.
44Aligeuza mito yao kuwa damu,
hawakuweza kunywa maji kutoka vijito vyao.
45Aliwapelekea makundi ya inzi wakawala,
na vyura wakawaharibu.
46Aliruhusu tunutu kuharibu mimea yao,
mazao yao kwa nzige.
47Aliharibu mizabibu yao kwa mvua ya mawe
na mikuyu yao kwa mvua iliyochangamana na theluji.
48Aliwaachia mifugo yao mvua ya mawe,
akayapiga makundi ya wanyama wao kwa radi.
49Aliwafungulia hasira yake kali,
ghadhabu yake, hasira na uadui,
na kundi la malaika wa kuharibu.
50Aliitengenezea njia hasira yake,
hakuwaepusha na kifo,
bali aliwaachia tauni.
51Aliwapiga wazaliwa wote wa kwanza wa Misri,
matunda ya kwanza ya ujana katika mahema ya Hamu.
52Lakini aliwatoa watu wake kama kundi,
akawaongoza kama kondoo kupitia jangwani.
53Aliwaongoza salama, wala hawakuogopa,
bali bahari iliwameza adui zao.
54Hivyo akawaleta hadi kwenye mpaka wa nchi yake takatifu,
hadi nchi ya vilima ambayo mkono wake wa kuume ulikuwa umeitwaa.
55Aliyafukuza mataifa mbele yao,
na kuwagawia nchi zao kama urithi,
aliwakalisha makabila ya Israeli katika makao yao.
56Lakini wao walimjaribu Mungu,
na kuasi dhidi ya Yeye Aliye Juu Sana,
wala hawakuzishika sheria zake.
57Kama baba zao, hawakuwa thabiti wala waaminifu,
wakawa wasioweza kutegemewa
kama upinde wenye kasoro.
58Wakamkasirisha Mungu kwa mahali pao pa juu pa kuabudia,
wakachochea wivu wake kwa sanamu zao.
59Mungu alipowasikia, alikasirika sana,
akamkataa Israeli kabisa.
60Akaiacha maskani ya Shilo,
hema alilokuwa ameliweka katikati ya wanadamu.
61Akalipeleka Sanduku la nguvu zake utumwani,
utukufu wake mikononi mwa adui.
62Aliachia watu wake wauawe kwa upanga,
akaukasirikia sana urithi wake.
63Moto uliwaangamiza vijana wao,
na wanawali wao hawakuimbiwa nyimbo za arusi,
64makuhani wao waliuawa kwa upanga,
wala wajane wao hawakuweza kulia.
65Ndipo Bwana alipoamka kama kuamka usingizini,
kama shujaa anavyoamka
kutoka bumbuazi la mvinyo.
66Aliwapiga na kuwashinda adui zake,
akawatia katika aibu ya milele.
67Ndipo alipoyakataa mahema ya Yusufu,
hakulichagua kabila la Efraimu,
68lakini alilichagua kabila la Yuda,
Mlima Sayuni, ambao aliupenda.
69Alijenga patakatifu pake kama vilele,
kama dunia ambayo aliimarisha milele.
70Akamchagua Daudi mtumishi wake
na kumtoa kwenye mazizi ya kondoo.
71Kutoka kuchunga kondoo alimleta
kuwa mchungaji wa watu wake Yakobo,
wa Israeli urithi wake.
72Naye Daudi aliwachunga kwa uadilifu wa moyo,
kwa mikono ya ustadi aliwaongoza.

Iliyochaguliwa sasa

Zaburi 78: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia