Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ufunuo 18:9-19

Ufunuo 18:9-19 NEN

“Wafalme wa dunia waliozini naye na kushiriki anasa zake watakapoona moshi wa kuungua kwake, watamlilia na kumwombolezea. Kwa hofu kubwa ya mateso yake, watasimama mbali na kulia na wakisema: “ ‘Ole! Ole, ee mji mkubwa, ee Babeli mji wenye nguvu! Hukumu yako imekuja katika saa moja!’ “Wafanyabiashara wa dunia watalia na kumwomboleza kwa sababu hakuna anunuaye bidhaa zao tena: Bidhaa za dhahabu, za fedha, za vito vya thamani na vya lulu, kitani safi, nguo za rangi ya zambarau, hariri, nguo nyekundu, aina zote za miti ya udi, na vifaa vyote vya pembe za ndovu, vifaa vyote vya miti yenye thamani kuliko yote, shaba, chuma na marmar, bidhaa za mdalasini, vikolezi, za uvumba, manemane, na uvumba wenye harufu nzuri, za divai, na mafuta ya zeituni, za unga mzuri na ngano; ngʼombe na kondoo; farasi na magari; na miili na roho za wanadamu. “Watasema, ‘Yale matunda ambayo roho yako iliyatamani yamekoma. Utajiri wako wote na fahari yako vimetoweka, wala haviwezi kupatikana tena kamwe!’ Wale wafanyabiashara waliotajirika kwa bidhaa hizo kutoka kwake watasimama mbali naye kwa hofu kubwa ya mateso yanayompata. Watalia na kuomboleza wakipiga kelele wakisema: “ ‘Ole! Ole, ee mji mkubwa, uliyekuwa umevikwa mavazi ya kitani safi, ya rangi ya zambarau na nyekundu, ukimetameta kwa dhahabu, vito vya thamani na lulu! Katika muda wa saa moja utajiri wote mkubwa kama huu umeangamia!’ “Kila nahodha, na wote wasafirio kwa meli, na wote wapatao kipato chao kutokana na bahari, watasimama mbali. Watakapouona moshi wa kuungua kwake watalia wakisema, ‘Je, kulipata kuwako mji mkubwa kama huu?’ Nao watajirushia mavumbi vichwani mwao, huku wakilia na kuomboleza, wakisema: “ ‘Ole! Ole, ee mji mkubwa, mji ambao wote wenye meli baharini walitajirika kupitia kwa mali zake! Katika saa moja tu ameangamizwa!