Ufunuo 21:9-14
Ufunuo 21:9-14 NEN
Mmoja wa wale malaika saba waliokuwa na yale mabakuli saba ya hayo mapigo saba ya mwisho akaja akaniambia, “Njoo, nami nitakuonyesha bibi arusi, yaani, mke wa Mwana-Kondoo.” Naye akanichukua katika Roho hadi kwenye mlima mkubwa na mrefu, akanionyesha ule Mji Mtakatifu, Yerusalemu, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu. Ulikuwa ukingʼaa kwa utukufu wa Mungu kama kito chenye thamani sana, kama yaspi, safi kama kioo. Ulikuwa na ukuta mkubwa, mrefu wenye malango kumi na mawili, pakiwa na malaika kumi na wawili kwenye hayo malango. Kwenye malango hayo yaliandikwa majina ya yale makabila kumi na mawili ya Israeli. Kulikuwa na malango matatu upande wa mashariki, matatu upande wa kaskazini, matatu upande wa kusini na matatu upande wa magharibi. Ukuta wa huo mji ulikuwa na misingi kumi na miwili, na juu yake yaliandikwa majina ya wale mitume kumi na wawili wa Mwana-Kondoo.